Friday, 21 July 2017

SERIKALI YATOA JIBU HILI KWA SHIRIKA LA ETHIOPIA KUTUMIA JIA LA NGORONGORO


BODI ya Utalii Nchini (TTB), imesema hatua ya Shirika la Ndege la Ethiopia kuweka jina la Ngorongoro kwenye ndege zake ni kuutangaza utalii wa Tanzania kama walivyokubaliana.


Ofisa Uhusiano Mkuu wa TTB, Geofrey Tengeneza, alisema jana kuwa shirika hilo limeingia makubaliano na bodi hiyo kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania ili kuvutia watalii wanaotaka kutembelea maeneo hayo.

“Kuna picha inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha moja ya ndege za shirika la ndege la Ethiopian Airlines ina jina la Ngorongoro, wala Watanzania tusiwe na wasiwasi sababu tayari kuna baadhi ya watu wanasema shirika hilo linapotosha ulimwengu kwa kusema Ngorongoro ni sehemu ya Ethiopia.

“Nawafahamisha Watanzania kuwa tuliingia mkataba au makubaliano kati ya TTB na Ethiopian Airlines kutangaza vivutio vya kiutalii vilivyopo Tanzania. Hivyo kuonekana kwa ndege yenye jina la Ngorongoro ni utekelezaji wa makubaliano hayo, si ndege hiyo tu ipo nyingine imeandika jina la Kilimanjaro,” alisema.

“Si kweli kuwa Mlima Kilimanjaro na hifadhi ya Ngorongoro vipo Ethiopia. Tusichukulie kila kitu kwa mtazamo hasi, vingine vina manufaa kwetu. Jina la Ngorongoro likiwapo hapo maana yake wao wana uwezo wa kuwapeleka watalii katika kivuti hicho.”

Alibainisha kuwa kuna baadhi ya mambo yanachuliwa kwa chuki kutokana na baadhi ya nchi jirani zilizokuwa zikitumia nafasi ya ukimya waliokuwa nao Watanzani katika kujitangaza kimataifa, hivyo kinachoendelea sasa ni kutumia fursa ya kujitangaza kwenye shirika hilo linaloingiza watalii wengi katika sehemu mbalimbali za dunia.

“Niwakumbushe tu ndugu zangu Watanzania kuwa hata shirika la ndege la KLM lipo jina limeandikwa Kilimanjaro je ni kweli Mlima Kilimanjaro uko Uholanzi,” alihoji,

Alisema kinachofanywa na shirika hilo ni kuutangaza mlima na kuwavutia abiria.

“Vitu hivyo vinafanyika maeneo mengi duniani. Hata Uingereza kuna bidhaa zina majina kama Kilimanjaro. Je, tuseme Mlima Kilimanjaro uko Uingereza? Na hata hapa Tanzania kuna maeneo au bidhaa zimepewa majina ya nje je, vitu hivyo vipo hapa nchini?

“Tukumbuke Ethiopia si washindani wetu katika vivutio vya kiutalii. Wao wamejipambanua zaidi katika vivutio vya kiutamaduni,” alisema.

TTB imekuwa sehemu ya mabadiliko yanayofanyika katika vivutio vya kiutalii kwa kutumia kila fursa iliyopo kuhakikisha Tanzania inatambulika kimataifa na watalii wanaongezeka kadiri iwezekanavyo.

Katika miezi ya hivi karibuni ardhi ya Tanzania imekuwa kivutio kikubwa katika nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwa kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani, wageni hao baadhi ni wasanii, wanamichezo, wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa waliokuja kutembelea vivutio vya kiutalii hasa mbuga za Serengeti na Ngorongoro.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive