Friday, 21 July 2017

ONYO LA JPM LAWAPA HOFU ACACIA


NI kiwewe kipya! Onyo alilolitoa Rais John Magufuli la kutaifisha migodi ya dhahabu na kuwapa wazawa ikiwa kampuni zilizowekeza zitachelewesha mazungumzo na serikali kuhusiana na upotevu wa mapato ya nchi kiasi cha matrilioni ya fedha, limezua hofu ya aina yake.


Akihutubia mamia ya wananchi mkoani Kigoma jana wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya kutoka Kibondo hadi Nyakanazi, Rais Magufuli alisema ataifunga migodi inayomilikiwa na wawekezaji wa kigeni na kuwapa wazawa endapo mazungumzo baina ya serikali na kampuni ya Barrick Gold kupitia mshirika wake, Acacia, yatachelewa.

Juni 14, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick, Prof. John Thornto, ambayo ndiyo mmiliki mkubwa wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia.

Kwenye mazungumzo yao, kwa mujibu wa Rais Magufuli, wamiliki wa kampuni hiyo walikubali kufanya mazungumzo na serikali ili kulipa fedha ambazo Tanzania imepoteza tangu kampuni hiyo ianze kuendesha shughuli zake nchini.

Acacia inayomilikiwa na Barrick, ndiyo yenye migodi iliyokuwa ikisafirisha makinikia kwa kiasi kikubwa ambayo ni ya Bulyanhulu na Buzwagi. Mgodi mwingine wa kampuni hiyo nchini ni North Mara, ambao hata hivyo huwa hauzalishi makinikia.

Hivi karibuni, kamati teule mbili alizounda Rais Magufuli kuchunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi zilibaini tofauti kubwa ya taarifa kati ya kile kilichokuwamo ndani ya makontena 277 yaliyozuiwa bandarini na kilichokuwa kikirekodiwa, hali iliyokuwa ikiikosesha serikali mapato yaliyotajwa kufikia kiasi cha matrilioni ya shilingi.

Jana, vyanzo viliiambia Nipashe kuwa baada ya onyo la Rais Magufuli, hofu ilitanda hasa kwa baadhi ya wafanyakazi wa Acacia kuhusiana na hatma ya migodi hiyo.

“Hili onyo alilotoa Rais limezua mshituko mkubwa. Ni wazi kwamba baada ya ujumbe huu uongozi wa Barrick utaongeza kasi ya kukaa na serikali ili kushughulikia mgogoro uliopo na hatimaye kuepusha hatua hizo kali zaidi za serikali,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana, huku kikitaja wadau wengine walioingiwa kiwewe kuwa ni pamoja na watu wanaofanya biashara na migodi iliyo chini ya Barrick pamoja na wafanyakazi.

Nipashe ilipowauliza Acacia jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na onyo hilo la Rais Magufuli, ufafanuzi uliotolewa uliashiria kuwa bado wana matumaini makubwa na kuanza kwa mazungumzo hayo ili mwishowe kufikia muafaka.

“Wakati majadiliano hayo yakiwa bado hayajaanza, tunaelewa kwamba yataanza hivi karibuni na yatalenga kufikia azimio mapema iwezekanavyo (kuhusiana na) mgogoro uliopo,” alisema msemaji wa Acacia.

Aidha, wakati Rais Magufuli akitoa onyo hilo, jana Acacia walitoa taarifa yao ya fedha pia kwa kipindi cha miezi sita kilichoishia Juni 30, 2017 na muhtasari wake kuwekwa kwenye tovuti yao.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa kuna upungufu wa fedha kiasi cha dola za Marekani milioni 175, chanzo kikielezwa bayana kuwa ni changamoto zitokanazo na zuio la usafirishaji makinikia nchini Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, alikaririwa akisema katika taarifa hiyo kuwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha imekumbwa na changamoto kubwa katika uendeshaji nchini Tanzania kutokana na kuanza kwa zuio la usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) kuanzia Machi, lakini kwa ujumla hali ilikuwa ya kuridhisha.

Gordon alitaja tofauti hiyo ilivyopatikana kwa kutaja anguko la urari wa fedha kutoka dola za Marekani milioni 318 hadi milioni 176.

Alisema walishindwa kuingiza kiasi cha dola milioni 175 na ziada nyingine ya dola za Marekani milioni 51 itokanayo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Hata hivyo, kwa ujumla, taarifa hiyo ya Gordon ilieleza kuwa licha ya changamoto zilizopo na ambazo wanatarajia zitapatiwa ufumbuzi kwa njia ya maridhiano, Acacia iliandika historia katika uzalishaji wake kwa kipindi kama hicho baada ya kuzalisha dhahabu ya kiasi cha aunsi 428,203.

UNDANI ONYO LA JPM
Akizungumza na wananchi mjini Kigoma, Rais Magufuli alisema anafahamu matrilioni ya fedha yalivyoibwa kwenye sekta ya migodi.

“Kwa sasa tumewaita wafanye mazungumzo na wamekubali, lakini wakichelewa nitafunga migodi yote na kuwakabidhi Watanzania… ni mara 10 migodi hii tukaigawa kwa Watanzania wachimbe wauze ili tupate kodi kuliko hawa wawekezaji ambao hawalipi kodi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Tanzania ni tajiri lakini tumechezewa sana. Niko serikalini, hivyo najua siri za serikali. Tumechezewa sana kwa kuibiwa rasilimali zetu. Kwenye dhahabu tumeibiwa mno. Ukiyajua yaliyokuwa yanafanyika unaweza kulia… unaweza kutamani usiishi.”

Alisema kuna Watanzania ambao serikali iliwaamini na kuwapa nafasi ya kushirikiana na wawekezaji ambao walikuwa wakidai kuwa kinachosafirishwa ni mchanga na si dhahabu na akahoji kama ni mchanga tu, mbona hawajawahi kwenda kuchukua mchanga Kibondo.

“Tuliwaamini wakaupakia kwenye makontena, wakaupeleka Ulaya. Wakiusafisha mbona hawaurudishi kama ni mchanga. Ulikuwa utapeli wa ajabu. Ni aibu kubwa kuona hili lilikuwa linafanywa na watu wakubwa… ni dharau kubwa kwa taifa maskini.

Watu wanakufa wanakosa maji, barabara, wanakufa kwa kipindupindu, hawapati elimu bora, umeme,” alisema Rais Magufuli, akionyesha wazi kuendelea kuumkizwa na hali hiyo .

Alisema wawekezaji hao walikuwa wanasomba rasilimali hizo bila kujali utu wa Watanzania na kuongeza kuwa yeye amezaliwa kwa ajili ya Watanzania na kwamba kama kuna baya lolote ni heri limtokee kwa kuwa yote anayoyafanya anayafanya kwa manufaa ya Watanzania.

“Nimeanzisha vita ya kiuchumi. Najua ni vita mbaya sana. Wakubwa wale huwa hawafurahi. Kuna viongozi wengi tumeona yaliyowapata kwa sababu nchi zao zilikuwa na mali lakini wale wakubwa walitaka kuzichezea kwa manufaa yao badala ya kuwanufaisha wananchi. Lakini naamini Mungu wangu ni mwema,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwashangaa wale wanaotetea wezi na kuwaita kuwa ni ‘mawakala wa shetani’.

ONGEZEKO LA KODI

Akizungumzia mapato, alisema alipoingia madarakani, makusanyo ya kodi yalikuwa kati ya Sh. Bilioni 800 na Sh. 850 lakini alivyobana mianya ya ukwepaji kodi, sasa yamepanda hadi Sh. trilioni 1.2 mpaka trilioni 1.3, huku akiongeza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikibana zaidi inaweza kupata hadi trilioni mbili na zaidi.

“Fedha nyingi serikalini zinavuja kutokana na matumizi mabaya. Unakuta watu wanatembea kila mahali semina, mikutano, posho na safari. Sasa hivi safari mpaka nikupe ruhusa. Hizo ndizo pesa za wananchi zilivyokuwa zikichezewa,” alisema.

Aidha, alisema fedha za dawa zimeongezeka, serikali imenunua vitanda vya hospitali, vifaa vya maabara vya shule ambavyo vitaanza kugawiwa na kuongeza shule za kidato cha tano na sita.

“Tuna Waziri mchapakazi katika Wizara ya Elimu (Profesa Joyce Ndalichako). Alitaka kugombea ubunge ila akasita kuwa mtamnyima kura. Ila nimempa uwaziri. Kuna Dk. Mpango, naye nilitaka agombee lakini akasita… lakini nikampa ubunge na kumteua kuwa Waziri wa Fedha (na Mipango) zote za Tanzania,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive