BAADA ya uongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutangaza kuachana na kiungo wake, Haruna Niyonzima kutokana na kushindwa kumpa kiasi cha fedha alichohitaji ili kusaini mkataba mpya, zimebaki saa 24 kitendawili cha Mnyarwanda kuteguliwa.
Taarifa kutoka Rwanda zinasema kuwa kwa sasa Niyonzima anashiriki kozi maalumu ya ukocha ya ngazi ya leseni C inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambayo inatarajiwa kumalizika ifikapo Julai 30 mwaka huu.
Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba inaeleza kuwa tayari maandalizi ya kiungo huyo Mnyarwanda kuelekea Afrika Kusini kuungana na wachezaji wenzake yameshafanyika na anatarajiwa kuungana nao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa licha ya Yanga kutangaza kushindwa kumshawishi nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) na kumtakia kheri katika maisha yake mapya, inaelezwa kwamba bado ujumbe maalumu unaendelea kumshawishi nyota huyo asaini mkataba mpya.
Hata hivyo viongozi wa Simba bado wamekuwa kimya kuhusiana na usajili wa Niyonzima kwa kuheshimu taratibu na kanuni zilizopo ili kuepuka kutozwa faini kama ilivyotokea kwa Yanga walivyomsajili beki Hassan Kessy mwaka jana.
"Siasa zimeingia kwenye usajili wa Niyonzima, ila naweza kukueleza kuwa asilimia 95 atatua Msimbazi na asilimia 5 atabaki Yanga," kilisema chanzo chetu.
Kiongozi mwingine wa Simba aliliambia gazeti la Nipashe kuwa sababu ambayo inamchelewesha Mganda Emmanuel Okwi kujiunga na wenzake ni kuchelewa kupata viza ya kuingia Afrika Kusini.
"Alikuwa na ruhusa ya kukamilisha mambo yake ya kifamilia, lakini sasa tunashughulikia viza yake, Waganda ni tofauti na sisi (Watanzania) ambao tunaingia Afrika Kusini bila kufanya maombi ya viza, ila tunaamini wiki ijayo kikosi kitakuwa kimekamilika," aliongeza kiongozi huyo.
Wakati huo huo taarifa kutoka Afrika Kusini zinasema beki Mohammed Hussein 'Tshabalala' atapata matibabu maalumu ya mguu alioumia kwenye fainali ya Kombe la FA iliyofanyika Dodoma na inaelezwa kuwa anaendelea vyema.
0 comments:
Post a Comment