Saturday, 22 July 2017

DCI BOAZ ATOA SIRI


Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz ametoboa siri ya mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kuripoti kwa mara ya nne ofisini kwake kwa tuhuma za uchochezi.



Boaz alisema si kwamba mara zote Lowassa anapo ripoti polisi huhojiwa, bali ni sehemu ya hatua za kukamilisha uchunguzi.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Boaz alisema kuhojiwa kwa mwanasiasa huyo kunatokana na utaratibu unaohitaji kujiridhisha na tuhuma hizo kabla ya kukamilisha upelelezi.

“Ni sehemu ya upelelezi, ziko hatua nyingi na siwezi kutoa ‘time frame’ (muda) ya kukamilisha uchunguzi, ndiyo maana tumetoa kipindi cha wiki tatu hivi ili kujiridhisha na kauli aliyotoa, uchunguzi unahitaji kuchukua taarifa hapa na pale ili kujua kesi sahihi ipo? Ili apelekwe mahakamani,” alisema Boaz.

Waziri Mkuu huyo wa zamani, juzi alifika makao makuu ya polisi saa 2:55 asubuhi na kuruhusiwa kuondoka saa 3:20 asubuhi.

Anatuhumiwa kutoa kauli ya uchochezi Juni 23 wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kuhusu masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) walio mahabusu kwa miaka minne sasa wakikabiliwa na kesi ya ugaidi, akitaka utaratibu wa kisheria ufuatwe.

Awali, wakili wa Lowassa, Peter Kibatala alisema baada ya kumalizika kwa mahojiano ya jana, mteja wake alitakiwa kuripoti katika tarehe atakayojulishwa baadaye.

“Sisi tumeitikia wito na tumefika lakini wanasema (Jeshi la Polisi) bado hawajakamilisha utaratibu wa uchunguzi kwa hiyo tumekubaliana ndani ya wiki tatu watakuwa tayari, tunaweza kupangiwa tarehe kabla ya wiki tatu kumalizika, watatupatia taarifa,” alisema Kibatala.

Alisema wako tayari kuendelea kuitikia wito wa jeshi hilo.

Kwa mara ya kwanza, Juni 27 Lowassa aliitikia wito wa kufika makao makuu ya Jeshi la Polisi ambako alihojiwa kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana na alitakiwa kurejea Juni 29 na alipokwenda alipangiwa kufika Julai 13 ambako alipangiwa kuripoti tena jana.

Jana, Lowassa alifika makao makuu ya jeshi hilo akiwa ameambatana na mkewe Regina na wasaidizi wake, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.

Askari waliokuwa eneo hilo waliwazuia waandishi wa habari kuingia ndani ya jengo hilo.

Maoni ya wachambuzi

Baadhi ya wanasheria walihojiwa kuhusu suala hilo na mmoja wao, wakili wa kujitegemea, Onesmo Mpinzile alizungumzia muda wa kufanyika upelelezi alisema ni vigumu kutambua muda sahihi wa uchunguzi.

Alisema muda wa uchunguzi unategemea aina ya tuhuma. “Inategemea ni nini Polisi wanachunguza na hawawezi kusema kwa kuwa wanaweza kuathiri uchunguzi wao, pengine wanachunguza maelezo aliyoyatoa au wanachunguza kauli kama zinatofautiana, kama alitoa kwa nia njema au la. Aina ya tuhuma hutofautiana na muda utakaotumika,” alisema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala Bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari alisema kauli aliyotoa Lowassa ni haki ya kikatiba kwa Mtanzania yeyote kuhoji hisia zake pale anapoona jambo linatia shaka.

“Nadhani hakuzungumza kwa nia mbaya ila alitoa wasiwasi wake, raia yeyote ana haki kutoa maoni pale anapoona kunatia shaka, si kuingilia uhuru wa Mahakama,” alisema.

Profesa Bakari alisema kinachoendelea kwa sasa barani Afrika na nchi zingine ikiwamo Tanzania ni mkakati wa kudhoofisha nguvu ya vyama vya upinzani kupitia tuhuma za kesi za uchochezi.

Alisema lengo ni kuwafungulia mashtaka wanasiasa wa vyama vya upinzani ili kuwavunja nguvu ya kuendelea na kazi za kisiasa, mbinu aliyosema kwa karne ya sasa haiwezekani.

“Ukiangalia Zimbabwe vyama vya upinzani wanakutana na changamoto kama hii inayojitokeza Tanzania, pia Uganda wapinzani wanapata wakati mgumu kwa kufunguliwa mashtaka, kuwekwa mahabusu, lakini strategy hizo zilifanikiwa miaka 1960, 1970 lakini si kwa zama hizi wananchi wanauelewa mkubwa wa kuhoji,” alisema.

Profesa Bakari alisema hali hiyo inaharibu mtangamano wa kisiasa nchini kwa kuwa haipendezi kuona siasa za vikwazo katika Taifa lenye misingi ya kidemokrasia na sifa ya kuwa na amani.

Hata hivyo, Boaz alisema suala hilo lisihusishwe na mambo ya kisiasa.

“Polisi haifungamani na siasa, sisi tunatafuta ukweli wa jambo, inawezekana uchunguzi ukachukua muda mrefu au mfupi, inategemea unafanya uchunguzi gani na katika mazingira yapi, isihusishwe na siasa ila sisi tunaangalia facts,” alisema.

Kuhusu haki ya kikatiba katika uhuru wa kutoa maoni aliyotoa Lowassa, Boaz alisema uchunguzi ndiyo utakaokuwa na majibu katika hilo.     
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive