TAARIFA za ujio wa kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima
ndani ya Simba zimemkosha kocha wa timu hiyo, Joseph Omog raia wa
Cameroon ambapo ameweka wazi ya moyoni kuwa nyota huyo atawasaidia msimu
ujao.
Niyonzima anadaiwa kumalizana na viongozi wa Simba kwa ajili ya
kukichezea kikosi hicho kilichopo nchini Afrika Kusini katika msimu ujao
wa 2017/18 akitokea kwa wapinzani wao, Yanga.
Kocha huyo aliyeipa ubingwa wa FA Simba msimu uliopita, ameliambia Championi Jumatatu kuwa,
kama kweli kiungo huyo anajiunga nao basi Simba itatisha na itawatambia
wapinzani wao kwa msimu ujao kutokana na uwezo wake mkubwa hasa katika
kutengeneza nafasi za kufunga.
“Ikiwa kweli Niyonzima anatua kwetu basi nakwambia tutatisha sana
msimu ujao na wapinzani wetu wajiandae kuumia kwani kiungo huyo ni moja
ya wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na hakuna kocha ambaye
atakataa kuwa naye kwenye kikosi chake.
“Kila mmoja anajua uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi zenye macho na
anapoongezeka ina maana kwamba washambuliaji wetu watakuwa wanapata pasi
nyingi za kufunga na kusababisha tuwe tunashinda katika michezo yetu
mingi.
“Kikubwa nasubiri kuona kama atatua maana mpaka sasa sijajua kama ni
kweli au la, lakini pia naendelea kukinoa kikosi changu kuhakikisha
kinakuwa na makali na kufanya vizuri kwenye mechi zake ikiwemo ya Simba
Day,” alisema Mcameroon huyo.
Katika maelezo yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe,
juzi alisema wameshazungumza na mchezaji huyo lakini hakufafanua zaidi
huku akisema kuna wachezaji wawili wanawataka na bado wana mikataba na
timu zao za zamani, hivyo hawawezi kuwataja kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa pia, Simba inatajwa kumalizana na Aishi Manula ambaye
pia bado ana mkataba na Azam FC lakini ameshaweka wazi kuwa ataondoka
klabuni hapo na inavyoonekana kuwa atatua Msimbazi pamoja na Niyonzima.
Mbona watakoma msimu huu.
ReplyDelete