Muumini wa kanisa Katoliki, Adrian
Mpande amepigwa risasi mbili akiwa anasubiri kuingia kanisani katika
Parokia ya Kibangu wilaya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa George Ng’atigwa ambaye
ni shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa Mpande alikuwa akisubiri kuingia
kanisani majira ya saa tatu asubuhi lakini alikuja mtu mmoja aliyekuwa
anatembea kwa miguu na kumpiga risasi ubavuni na mkononi, hali
iliyosababisha aanguke na kupoteza fahamu.
Alisema kuwa mtu huyo alikimbia
lakini watu waliokuwa maeneo hayo walifanikiwa kumkamata baada ya
kuishiwa risasi wakati akijaribu kuwatishia.
Aliongeza kuwa baada ya kumkamata mtu
huyo, waliwasiliana na jeshi la polisi ambalo lilifika na kuondoka naye
kwa ajili ya taratibu za kisheria na kwamba majeruhi alikimbizwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kupatiwa huduma ya kwanza
katika zahanati iliyokuwa karibu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa
Dar es Salaam, Suzan Kaganda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kueleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa limetokana na ugomvi wa
kifamilia.
“Mtuhumiwa tunaye tunaendelea
kumhoji na aliyejeruhiwa yuko hospitali anaendelea na matibatu katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” Kamanda Kaganda anakaririwa.
0 comments:
Post a Comment