Friday 28 July 2017

MABOSI WA YANGA WAFANYA MAAJABU WAMLETA NA HUYU TENA

WAKATI kiungo rasta, Tshishimbi Kabamba ‘Papii’ akisaini mkataba wa miaka miwili kuitumia Yanga, mabosi wa klabu hiyo wamefanya kitu kingine cha maana baada ya kumalizana na kiungo mwingine fundi.
Yanga imemsainisha kiungo Raphael Daud kutoka Mbeya City tayari kuitumikia klabu hiyo na leo Ijumaa timu inatarajiwa kutua kambini mjini Morogoro kuungana na wachezaji wenzao kwa maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.
Habari kutoka kwa mabosi wa Yanga, ni kwamba Rafael alisainishwa mkataba huo juzi Jumatano, lakini waliamua kufanya siri kwa sababu kuna mambo hawajamalizana na klabu yake ya City.
“Rasta amesaini tayari kuanza kuitumikia Yanga, lakini pia tumemalizana na kiungo Rafael Daud ambaye tulishaanza mazungumzo naye mapema, lakini ikawa bado kusaini kitu kilichokamilika juzi,” kilisema chanzo hicho makini.
Yanga ilikamilisha dili la Papii anayetokea Mbabane Swallows ya Swaziland, baada ya juzi kumfanyia vipimo vya afya siku chache tangu alipotua nchini ili kuja kumalizana na mabosi wa Yanga.
Papii alisaini mkataba huo mchana wa jana na kuifanya Yanga sasa kusaliwa na nafasi moja kwa nyota wa kigeni ambayo inawaniwa na Mnigeria Henry Tony Okoh na Mkameruni Fernando Bongyang.
Wachezaji hao wawili wa kigeni kwa sasa wanaendelea kwa ukaribu na Kocha George Lwandamina kabla ya kutoa maamuzi yupi amwage wino, japo Mnigeria anapewa nafasi kubwa kwa aina yake ya uchezaji.
Mandawa asaini BDF
Katika hatua nyingine, straika Rashid Mandawa aliyekuwa Mtibwa Sugar amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu ya BDF XI  ya Ligi Kuu Botswana.
Mandawa aliyewahi kung’ara Kagera Sugar, Mwadui na Taifa Stars, amesaini mkataba huo baada ya kufuzu majaribio yake na kwamba ataanza kuitumikia timu hiyo iliyoshika nafasi ya nane katika Ligi Kuu Bostwana msimu uliopita.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive