Monday, 10 July 2017

KENYATA APUNGUZIWA MSHAHARA...


Image result for kenyatta

Tume ya mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma nchini Kenya imetangaza kupunguzwa kwa mishahara ya maafisa wakuu wakiwemo rais na wabunge.


Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Sarah Serem ametoa mpangilio mpya wa malipo ambao anasema utaokoa jumla ya Sh8 bilioni (dola 80 milioni za Marekani) kila mwaka na kupunguza jumla ya mishahara inayolipwa watumishi wa umma kwa asilimia 35 .

Tume hiyo imependekeza kufutiliwa mbali kwa marupurupu ya kipimo cha usafiri wa magari kwa magavana na wabunge na badala yake hilo litakuwa likifidiwa na mfumo mpya wa marupurupu kwa kuzingatia kanda.

Rais sasa atakuwa akilipwa Sh1.4 milioni (dola 14,000) kila mwezi badala ya Sh1.65 milioni (dola 16,500), naye naibu wake awe akilipwa Sh1.2 milioni (dola 12,000).

Mawaziri watakuwa wakilipwa Sh924,000 (dola 9,200), Spika wa Bunge Sh1.1 milioni (dola 11,000) nao magavana wa kaunti Sh924,000 (dola 9,240).

Mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa tarehe 8 Agosti, 2017.

Bi Serem amesema maafisa wa serikali walikuwa wakitumia vibaya mfumo wa marupurupu wa kupimiwa usafiri wa magari.

Badala yake, maafisa sasa watakuwa wakilipwa marupurupu ya kila mwezi ya usafiri kwa kutegemea eneo anamotoka afisa husika.

Magavana na manaibu wa magavana pia hawatakuwa wakilipwa tena marupurupu.

Wabunge, ambao wamekuwa wakilipwa marupurupu kwa kuhudhuria vikao vya kamati mbalimbali, pia watakosa marupurupu hayo.

Viongozi wa serikali ya upinzani bungeni, ambao pia walikuwa wakipokea marupurupu ya majukumu maalum pia hawatalipwa tena marupurupu hayo.

Mishahara hiyo mipya itaanza kutekelezwa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti.

Maafisa ambao mihula yao haitakuwa imemalizika mwaka huu wataendelea kupokea mishahara yao ya awali.

Hata hivyo, watakaorithi nyadhifa hiyo watalipwa kwa kufuata utaratibu mpya.

Mishahara mipya:

Rais: Sh1.4 milioni kutoka Sh1.65 milioni

Naibu Rais: 1.2 milioni kutoka 1. 4 milioni

Mawaziri: Sh924,000 kutoka Sh1.056 milioni

Makatibu wa Wizara: Sh765,000 kutoka Sh874,000

Magavana: Sh924,000 kutoka Sh1.056 milioni

Wabunge: Sh621,000 kutoka Sh710,000

Maspika: Sh1.155 milioni kutoka Sh1.30 milioni

Naibu Spika: Sh924,000 kutoka Sh1.006 milioni

Viongozi wa Serikali na Upinzani Bungeni: Sh765,000 kutoka 1.020 milioni

Madiwani (Wawakilishi wa Wadi): Sh144,000 kutoka Sh165,000

Mawaziri wa Serikali za Kaunti: Sh259, 875 kutoka Sh350,000
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive