Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema kuwa ipo haja ya kuzalisha
wataalamu zaidi ili kukwepa kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Amesema hayo leo Jumatatu, Julai 24, alipokuwa akizindua mkutano wa siku
mbili uliozikutanisha nchi 12 zikiwamo za Afrika ili kujadili utoaji wa
huduma za afya hususani katika sekta binafsi.
Amesema katika majukwaa ni rahisi kusema hakuna haja ya kupeleka
wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu, lakini kiuhalisia
jambo hilo haliwezekani kwa sababu wataalamu waliopo ni wachache.
Ametolea mfano nchi nzima kuna wataalamu watatu wa upasuaji wenye
utaalamu wa mishipa ya fahamu ambao hawatoshi ukilinganisha na idadi ya
Watanzania wanaofikia 50 milioni.
Rais Kikwete pia alitumia mkutano huo kuwaasa wahudumu wa afya wa sekta
binafsi kusisistiza matumizi ya bima ya afya kwa wananchi badala ya
kung'ang'ania kudhaminiwa na Serikali kupata mikopo.
Amesema rais huyo mstaafu: "Msijisumbue kwa hili Serikali haiwezi
kuwadhamini wala msijidanganye, haiwezi kufanya hivyo kwa sababu
italazimika kutumia kodi za wananchi kulipa mikopo iliyowashinda kulipa.
“Wananchi wakiwa na bima ya afya mnaweza kujipanua hadi mikoani na
mkafanya kazi na kuacha kufanya mijini pekee ambako wananchi angalau
wanaweza kumudu gharama za matibabu," amesema.
Naye Mkurugenzi wa Mfuko wa Mikopo-Afrika Mashariki Evelyne Gitonga
amesema asilimia 84 ya vituo vya afya binafsi nchini Tanzania havifanyi
vizuri kutokana na kukosa ruzuku kutoka serikalini na kutofikiwa na
mikopo.
Amesema kukosekana mikopo na fedha za kujiendesha husababisha kutoa
huduma chini ya kiwango hali inayosababisha wanaovitegemea kuendelea
kuteseka.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa
wataalamu wanazalishwa kwa wingi changamoto iliyopo ni ajira.
Amesema wanalifanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha wanakuwa na
rasilimali watu ya kutosha ili kufanikisha azma ya utoaji huduma bora ya
afya.
0 comments:
Post a Comment