MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe
amekiri kuitwa kisha kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa Tanzania (Takukuru) ila hakushikiliwa kama ilivyoelezwa.
Juzi jioni baada ya Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kupelekwa mahabusu kwa makosa nane ikiwemo kutakatisha fedha, uvumi ulizagaa kukamatwa kwa Hans Poppe pia.
Akizungumza na moja kati ya vyombo vya habari hapa nchini Hans Poppe
alisema; “Kwanza nianze kwa kukiri kuwa niliitwa kuhojiwa na Takukuru,
niliitikia wito kwa kwenda, nikahojiwa na baadaye nikaondoka.
“Siyo kwamba ninashikiliwa kama inavyotangazwa, kuhusiana na kuhojiwa
tayari nilihojiwa kama mara mbili hivi kabla, hali hiyo ni ya kawaida
ambayo inaweza kumtokea mtu yeyote.
“Ni kama ilivyotokea kwa rais na makamu wetu, waliitwa kuhojiwa lakini baadaye wakalepekwa
mahakamani kisha kupelekwa mahabusu, ila mimi sikupelekwa mahakamani walianiachia palepale.”
Aveva na Kaburu watafikishwa tena mahakamani Julai 13, mwaka huu kuendelea na kesi zinazowakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
Wakati huohuo, Kamati ya Utendaji ya Simba inakutana leo Jumamosi
katika kikao cha dharura ili kujadili mustakabali wa Aveva na Kaburu
waliopo mahabusu.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully, alisema: “Sasa
klabu inajiendesha bila ya kuwa na viongozi wake wawili wakubwa, hivyo
tutakutana Jumamosi (leo) ili kupata watu watakaokaimu nafasi zao.”
0 comments:
Post a Comment