SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) muda wowote kuanzia sasa
litatuma maofisa wake kuja nchini kufuatilia tuhuma za utakatishaji
fedha alizonazo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Malinzi na wenzake ambao ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na
Mkurugenzi wa Fedha wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga walipandishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa 28 yakiwemo ya
utakatishaji fedha.
Baada ya kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbord
Mashauri katika kesi yao namba 213, watuhumiwa hao walinyimwa dhamana na
kupelekwa mahabusu hadi kesi yao itakaposikilizwa tena keshokutwa
Jumatatu.
Akizungumza na na moja kati ya vyombo vya habari hapa nchini, Makamu wa Rais wa
TFF, Wallace Karia alisema Fifa tayari ina taarifa za viongozi hao wa
TFF kukamatwa na kupandishwa kizimbani kisha kwenda mahabusu.
“Fifa itatuma maofisa wake muda wowote kuanzia sasa na wakifika
nchini tutakutana nao katika kikao Jumanne ijayo ili waweze kujua undani
wa tuhuma zote walizonazo wenzetu, nadhani kila kitu kitakuwa sawa
baada ya hapo.
“Sisi kama TFF hatuwezi kuzungumza lolote kuhusu kukamatwa kwa watu
hawa kwani tayari shauri lipo mahakamani,” alisema Karia ambaye pia
anagombea nafasi ya urais wa TFF katika uchaguzi utakaofanyika Agosti
12, mwaka huu mjini Dodoma.
Ni wazi kwamba kuna ugumu wa Malinzi kuwahi usaili kwani leo ndiyo mwisho na yeye atafikishwa mahakamani keshokutwa Jumatatu.
Hata hivyo, jana mchana zilivumishwa habari za rais huyo kuwasilisha
barua kwa kamati ya uchaguzi ya kuomba udhuru wa kutofanya usaili katika
siku zilizopangwa ili afanyiwe Jumatatu ijayo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli alikanusha uvumi huo jana jioni.
0 comments:
Post a Comment