
Leo June 22, 2017 Rais Magufuli amekamilisha
ziara yake ya kikazi siku tatu katika Mkoa wa Pwani ambako mbali na
shughuli nyingine, amezindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drink Ltd kabla ya kuzindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kumaliza kwa kuzindua mradi wa barabara ya Bagamoyo – Msata.
Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza kwenye Hotuba yake ni pamoja na
suala la elimu akisema Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kugharamia
elimu ambayo imeanza kutolewa bure kwa Watanzania wote.
“Nazungumza lingine ambalo
tumekuwa tukishughulikia. Tulipoingia madarakani ndugu zangu, na hili
nataka nilizungumze kwa sababu pamekuwa na yanazungumzwa mengi. Tuliamua
kutenga Bilioni 18.77 kwa ajili ya kutoa elimu bure. Kwamba mtoto
ataingia Darasa la Kwanza mpaka Sekondari asome bure.
“Na Serikali tunachukua Bajeti yetu katika hizi fedha
kidogo tunazozikusanya tunazipeleka kwenye elimu bure kwa sababu watoto
wetu – watoto wa Masikini walikuwa wanapata shida. Akienda shuleni
anaambiwa huna ada anarudi nyumbani baadaye hasomi.
“Tukasema hawa watoto wa
Masikini, watoto wa Watanzania lazima wasome bure. Sasa pametokea maneno
mengine siku hizi nawasikia wanazungumza sana kwamba watoto wanapoenda
Shule wakipata mimba akishatoka kuzaa arudi shuleni. Na unakuta hao
wanaozungumza sijui nao walipata mimba wakiwa shuleni?
“Nataka niwaeleze, tukienda kwa mzaha wa namna hiyo kwa
kusikiliza ma-NGOs yanakotupeleka yanalimaliza Taifa. Mtu ametoka pale
amepata mtoto, amezaa, iwe kwa makusudi, iwe kwa raha yake iwe kwa
bahati mbaya aende shuleni ameshazaa hawa wengine ambao hawajazaa, si
atawafundisha?
“Halafu akipata mimba tena
ya pili anaenda nyumbani akizaa tena anarudi shuleni. Anapata mimba ya
tatu anaenda nyumba akizaa anarudi shuleni, yaani tusomeshe wazazi?
“Nataka niwaambie, na hizi NGOs na nyinyi wote mnaosikia,
ndani ya utawala wangu kama Rais, hakuna mwenye mimba atakayerudi
shuleni. Narudia, hakuna mtu mwenye mtoto katika elimu hiyo ya Darasa la
Kwanza mpaka Sekondari atakayerudi shuleni.” – Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment