Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Juni, 2017
ameagana na wafanyakazi wa iliyokuwa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa
Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery Bureau – PDB) ambao
wamehamishiwa katika ofisi na taasisi nyingine za Serikali kwa ajili ya
kuendelea na utumishi wa umma.
Wafanyakazi hawa ndio walikuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN).
Mhe. Rais Magufuli amekutana na
wafanyakazi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo amewashukuru kwa kazi
nzuri waliyoifanya wakiwa PDB na amewataka kuendelea kulitumikia Taifa
kwa juhudi na maarifa wakiwa katika ofisi nyingine walizopangiwa.
“Natambua kuwa nyie ni wafanyakazi
wazuri wenye ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya Taifa letu. Mmetoa
mchango mkubwa mlipokuwa PDB nategemea mtaendelea hivyo na hata zaidi
katika ofisi mbalimbali mlizopangiwa, mkachape kazi kwa kutanguliza
maslahi ya Watanzania” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah
Kairuki, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Dkt. Laurian Ndumbaro.
Wakati huo huo, Mhe. Rais
Magufuli amekutana na timu ya wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa
miundombinu ya mabwawa ya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme na
kujadiliana nao kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji wa
umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project)
ambao una uwezo wa kuzalisha Megawatts 2,100 za umeme.
Mhe. Rais Magufuli amekutana na
wataalamu hao ikiwa ni utekelezaji wa nia yake ya kuhakikisha mradi huo
unaanza kujengwa haraka iwezekanavyo na kuzalisha umeme mwingi
utakaosaidia kuharakisha maendeleo hapa nchini, hususani ujenzi wa
viwanda.
“Kesho Waziri Mkuu wa Ethiopia
Mhe. Hailemariam Desalegn anawatuma wataalamu wake waliojenga mradi
mkubwa wa bwawa la maji la kuzalisha umeme kule Ethiopia, wakiwa hapa
mtakutana nao na mtabadilishana uzoefu, nataka na sisi tusichelewe,
tuzalishe umeme utusaidie kwenye ujenzi wa viwanda” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment