Waziri Mkuu
Mstaafu, Edward Lowassa amefunguka kuhusu alivyohojiwa kwa saa nne
katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambapo
baada ya kuhojiwa ameachiwa kwa dhamana na kuondoka makao makuu ya
polisi majira ya saa 8.
Akizungumza nyumbani kwake, Oyster Bay
jijini Dar mara baada ya kutoka Makao Makuu ya Polisi, Lowassa amesema
aliitwa kuhusu kauli aliyoitoa ya viongozi wa dini ya Kiislam wa
Zanzibar (Uamsho) kuendelea kusota rumande kwa miaka kadhaa sasa kauli
ambayo inadaiwa kuwa kuwa ni ya uchochezi.
“Nimeitwa kuhojiwa kuhusu hotuba
niliyoitoa hivi karibuni wakati wa futari kwa Mbunge Waitara. wengine
wameielewa kama ni ya uchochezi.
“Nimejieleza wachakuchua maelezo yangu ambayo wanayatafakari hivyo tutakutana tena Alhamisi saa 6:00 mchana.
“Hivyo niwatake wanachama wa Chadema wasiwe na hofu, tupo imara.” alisema Lowassa
Wakati wa futari iliyoandaliwa na
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) Lowassa alisema aliwaahidi
wananchi endapo angechaguliwa kuwa rais angewatoa mashehe hao siku hiyo
hiyo lakini anashangaa viongozi hao wa dini wanavyoendelea kusota
rumande mpaka sasa bila kufahamu kosa lao.
Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala
amesema Lowassa amejidhamini mwenyewe na ametakiwa kuripoti tena
Alhamisi saa 6.00 mchana.
“Mzee amehojiwa kwa kile wanachokiita kauli ya uchochezi aliyoitoa
Juni 23, mwaka huu wakati wa futari iliyoandaliwa na Waitara. Baada ya
kuhojiwa ameandika maelezo ya onyo na atatakiwa kuripoti tena Alhamisi,
Juni 29,” amesema Kibatala.
0 comments:
Post a Comment