SIKU chache baada ya Haruna Niyonzima na Donald Ngoma kudaiwa
kuondoka Yanga na kuwa mbioni kumalizana na Simba, beki kisiki Mtogo,
Vincent Bossou naye amewaita Wekundu hao wa Msimbazi akidai yupo tayari
kusaini mkataba katika kikosi chao kama wakimfuata.
Bossou aliyebeba makombe mawili ya Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga iliyo
chini ya Mzambia, George Lwandamina, mkataba wake unaelekea kumalizika,
jambo ambalo linamfanya awe mchezaji huru.
Akizungumza na moja ya vyombo vya habari hapa nchini kutoka Togo alipo
kwenye mapumziko baada ya kumalizika kwa ligi, Bossou amesema kuwa
kuhamia Simba kwake hakuna kitu kipya kwani maisha ya kimpira ndivyo
yalivyo kwa mchezaji yeyote kuhama.
“Bado sijazipata taarifa za Simba kutaka huduma yangu kwenye kikosi
chao kwa msimu ujao, lakini kama itakuwa kweli nawaambia kwamba waje
tuzungumze kwa sababu mkataba wangu na Yanga unaenda ukingoni hapa,
zimebaki siku chache pekee.
“Nikwambie tu kuwa hata kama itatokea nimehamia Simba kutakuwa hakuna
jambo jipya kwa sababu huo ndiyo mpira, unakuta leo mchezaji yupo hapa
kesho yupo kule, itategemea tu na maslahi utakayopewa,” alisema beki
huyo aliyeshiriki michuano ya Kombe la Afrika (Afcon) Januari, mwaka huu
akiwa na Togo.
0 comments:
Post a Comment