KIONGOZI wa ACT
Wazalendo na Mbunge wa Kigoma mjini, Mh. Zitto Kabwe amefunguka na
kusema kwamba uchungu anaoupata baada ya nyumba yake ya kwanza kuungua
moto umemfanya kuwafikiria wananchi wanaobomolewa nyumba zao bila fidia.
Zitto amebainisha hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook baada ya kutazama nyumba yake ya kwanza iliyoteketea kwa ajali ya moto mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Sikudhani kabisa kuwa naweza
kuumizwa na kupata uchungu kwa tukio kama hili na ninajiuliza huu
uchungu ni wa nini? Kumbe ni uchungu wa nyumba ya kwanza. Nawafikiria
wananchi wenzangu wanaobomolewa nyumba zao bila fidia, na wengi ni
nyumba zao za kwanza na pekee. Uchungu wao nausikia. Hasira zao
nazihisi,” Zitto ameandika.
Ameongeza kuwa “Nafikiria
wanaobomolewa maeneo ambayo yamekuwa sehemu ya maisha yao na kuwapa
kipato na familia zao. Nausikia uchungu wao. Sio uchungu wa nyumba ya
kwanza. Uchungu wa kupoteza kabisa walichonacho na pengine kupoteza
matumaini ya maisha.”
Pamoja na hayo Zitto amesema kuwa
ameridhika kwamba kilichotokea kwenye nyumba yake kuungua moto ni ajali
ya kawaida na wala watu wasichukulie kwa muktadha wa matukio
yanayoendelea nchini kwetu hivi sasa.
“Ni ajali na funzo ni kuchukua
tahadhari zaidi. Hasara ni kubwa sana lakini muhimu ni kuwa maisha
yanaendelea na Mungu ataleta uwezo wa kuendeleza mengine. Nilipata
salaam kutoka kwa watu wengi na napenda kuthibitisha kuwa ni ajali tu,” Zitto.
Mbali na hayo Mh. Zitto Kabwe amesema
kuwa nyumba yake imeungua siku moja baada ya yeye kuondoka Kigoma na
akiwa njiani kuelekea nchini Kenya ndipo alipatiwa taarifa kuhusu ajali
hiyo.
“Ajali imetokea siku moja tu baada
ya mimi kutoka Kigoma, Septemba 15 , 2017. Hata hivyo muda wote wa siku
2 nikiwa nje ya Kigoma, sikupata hisia kabisa. Labda ni kwa sababu ya
safari yangu ya Kenya ambayo nayo haikuwa ni kwa jambo la kawaida” Zitto.
Aidha Mh Zitto ameongeza “Leo
asubuhi nimeamka na kurudi kutazama nyumba hii. Imekwisha yote
nimezunguka zaidi ya mara 3 kutazama gofu lile lile nililotazama jana
baada ya kufika. Nimechungulia chumba nilichokuwa nalala zaidi ya mara
moja. Nipo kama mwendawazimu,” alisisitiza Zitto Kabwe.
Nyumba ya Zitto Kabwe iliyoungua huko
Mwandiga mkoani Kigoma inadaiwa ndiyo nyumba yake ya kwanza baada ya
kupata ridhaa ya kuwa mbunge
0 comments:
Post a Comment