Thursday 7 September 2017

OMOG AWASHTUA YANGA

NAMBA hazidanganyi. Kocha wa Simba, Joseph Omog ameonyesha kuwa siyo mtu wa mchezo mchezo baada ya rekodi kubainisha ndiye kocha mwenye wastani mzuri zaidi wa ushindi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
Jambo hilo linamlazimu Kocha wa Yanga, George Lwandamina na jopo lake kujipanga upya kwani hata aliyempokea kijiti hafikii rekodi hiyo.
Omog ambaye anafundisha timu za Ligi Kuu Bara kwa mara ya pili sasa, ameshinda asilimia 70 ya mechi zote za timu alizowahi kuzifundisha nchini ikiwemo wakati akiwa Azam FC na sasa Simba.
Kocha huyo raia wa Cameroon aliifundisha Azam kuanzia Desemba 2013 hadi Februari 2015 alipofungashiwa virago baada ya timu yake kuondoshwa katika michuano ya kimataifa na Al Merreikh ya Sudan.
Wakati Omog akipata alama hizo, makocha wengine wawili Hans Van Pluijm aliyekuwa Yanga na sasa Singida United na Lwandamina aliyepo Yanga sasa wanasubiri nyuma yake.
Lwandamina ndiye mwenye rekodi nzuri juu ya Pluijm baada ya kuiongoza Yanga kushinda asilimia 68.7 ya mechi alizoifundisha huku Pluijm akipata ushindi kwa asilimia 66 katika mechi zote za Ligi Kuu Bara alizowahi kuziongoza Yanga na Singida United.

Mataji
Wakati Pluijm akishika nafasi ya mwisho katika orodha ya mechi alizoshinda, rekodi zinaonyesha ndiye kocha aliyeshinda mataji mengi zaidi nchini kwa sasa.
Pluijm ana rekodi ya kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu na Yanga huku pia akitwaa taji moja la FA na mengine mawili ya Ngao ya Jamii jambo ambalo linamfanya kuwa namba moja.
Katika vita hiyo ya mataji, Pluijm anafuatiwa na Omog ambaye amewahi kushinda taji moja la Ligi Kuu, moja la FA na moja la Ngao ya Jamii aliloshinda baada ya kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kwa upande wa Lwandamina, licha ya kuwa nchini kwa muda mfupi ana rekodi ya kushinda taji moja la Ligi Kuu ambalo alitwaa na Yanga msimu uliopita. Lwandamina alilikosa Kombe la Mapinduzi, FA na Ngao ya Jamii ambayo Yanga imeshiriki ikiwa chini yake.

Pluijm vipigo vikubwa
Kwa upande wa makocha hao watatu, Pluijm ndiye kinara wa kupata ushindi mkubwa katika Ligi Kuu enzi zake akiwa Yanga alishuhudia timu yake ikipata ushindi wa mabao matano ama zaidi mara nane.
Yanga ilizifunga timu za Coastal Union 8-0, Ruvu Shooting 7-0 kisha 5-0, wakati Kagera Sugar ikipokea dhahama ya mabao 6-2.
 Timu nyingine zilizokumbana na kimbunga Pluijm ni JKT Ruvu na African Sports nazo zikipokea vipigo vya mabao 5-0 na 5-1.
Kwa upande wa Omog ameshinda mechi mbili tu kwa mabao matano ama zaidi ambapo akiwa Azam aliifunga Mtibwa Sugar mabao 5-2 Februari 2015 kisha kuifunga Ruvu Shooting kwa mabao 7-0 wiki moja iliyopita.
Kwa upande wa Lwandamina bado hajafanikiwa kupata ushindi wowote wa mabao matano ama zaidi licha ya kubeba ndoo msimu uliopita.

Pluijm mkwanja
Kwa upande wa kusaini mikataba minono, Pluijm ndiye anawakimbiza makocha hao wawili ambapo wakati akiwa Yanga alikuwa ndiye kocha anayelipwa ghali zaidi nchini akipokea Dola 10,000 (Sh22 milioni) kwa mwezi huku mshahara wake ukipanda hadi Dola 12,000 (Sh26.6 milioni) pindi alipopandishwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.
Lwandamina anafuatia kwa kupokea mkwanja mnene ambapo kwa mwezi analipwa Dola 7000 (Sh15.5 milioni) huku Omog alishika nafasi ya tatu kwa mshahara wa Dola 6,000 (Sh13.3 milioni).

Vita kali
Kwa msimu huu vita kali ya kuwania ubingwa iko miongoni mwa makocha hao watatu huku kocha mwingine, Aristica Cioaba wa Azam akitarajiwa kufanya maajabu ambayo pengine hayawezi kutarajiwa na wengi.
Omog tayari ameanza kwa kasi akiwafunika wenzake baada ya kupata ushindi wa mabao 7-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Ruvu Shooting wakati Pluijm alipokea kipigo cha mabao 2-1 ugenini dhidi ya Mwadui.
Lwandamina alianza na sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Lipuli wakati Cioaba alipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda ugenini, hivyo kuibua ushindani kuelekea katika vita ya ubingwa msimu
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive