KAMATI ya Bunge iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai
kuchunguza biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite imependekeza
wajumbe wote wa bodi na waliohusika na kusimamia mgodi wa madini hayo,
wahojiwe na ikibainika wamehusika na mapungufu wachukuliwe hatua.
Akisoma ripoti ya kamati hiyo ambayo imekabidhiwa kwa Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye naye ameikabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwenyekiti wa kamati hiyo, Mussa Zungu amesema wamebaini madudu mengi.
Madudu hayo ni pamoja na upotevu wa
kodi, kutosimamiwa vyema kwa uchimbaji wa madini hayo, tofauti kubwa
kati ya takwimu zinazotolewa na taasisi za Serikali juu ya kiasi
kilichopatikana na kuuzwa cha madini hayo na udanganyifu kuhusu hali na
gharama za mitambo.
“Serikali ihoji wajumbe wote wa bodi ya
migodi hiyo na wote wanaohusika na ikibainika kuwa walihusika katika
mapungufu waliyoyaona wachukuliwe hatua,” amesema.
Zungu ameeleza kuwa, Profesa Abdulkarim Hamis Mruma aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya kwanza iliyoundwa na Rais Magufuli
kuchunguza kiwango cha madini kwenye mchanga wa madini (Makinikia)
anadaiwa kuisababishia serikali hasara kupitia Almasi na Tanzanite akiwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Madini.
Amesema kuwa Mruma alikiri mbele ya
kamati kuwa alishindwa kufuatilia madeni yaliyobambikwa kwa serikali ya
Tanzania kwa sababu hakuwa na muda wa kusoma hivyo aliyapitisha madeni
hayo kwani aliwaamini waliompelekea taarifa hizo (watendaji wa wizara).
Aidha, Zungu amesema kuwa Kamati
imebaini kuwa waliokuwa Mawaziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo na
William Ngeleja walitoa leseni za madini kinyume na sheria huku Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Eng. Edwin Ngonyani akiwa STAMICO
alishindwa kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa ufasaha.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema
kuwa kesho saa 4:30 asubuhi atamkabidhi Rais Magufuli ripoti mbili za
uchunguzi wa biashara ya Almasi na Tanzanite alizokabidhiwa leo na Spika
Ndugai.
0 comments:
Post a Comment