Saturday 9 September 2017

MKUDE AMTOLEA UVIVU TSHISHIMBI

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude, ameibuka na kujinasibu kuwa, anayo dawa ya kumkabili kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi raia wa DR Congo pindi wakikutana uwanjani.

Mkude ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya Tshishimbi kuwa gumzo kutokana na kiwango chake kikubwa ambacho alianza kukionyesha kwenye mechi ya kwanza ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Katika mchezo huo ambao Mkude hakucheza huku Tshishimbi aking’ara kwenye nafasi ya kiungo na kuwakimbiza viungo wa Simba, Haruna Niyonzima na Mzamiru Yassin, Simba iliibuka na ushindi wa penalti 5-4.
Mkude kwanza alikiri Tshishimbi ni kiungo hatari, lakini akajinasibu kwamba akikutana naye uwanjani, basi atafanikiwa kumdhibiti vilivyo kwani dawa ya kufanya hivyo anayo.

“Kiukweli Tshishimbi ni kiungo mzuri ambaye anajua kucheza katika nafasi yake kwa ufasaha, nilimuona siku ile tulipocheza nao, aliweza kuwasumbua sana viungo wetu, lakini pale ningekuwa mimi, asingeweza kufanya vile.

“Mimi dawa yake ninayo, mtu kama yule hutakiwi kumkaba kwa macho, unatakiwa kumkuta kila anapokuwa na mpira, kucheza naye kibabe inaweza kukusaidia kumfanya asiwe na makeke uwanjani kwa sababu wachezaji wengi hawapendi kufanyiwa fujo wakiwa na mpira, basi ukimchezea hivyo mara kwa mara, muda mwingine akikuona anatoa pasi haraka,” alisema Mkude.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive