Klabu za Ligi Kuu ya England
ziliweka rekodi mpya ya kutumia pesa nyingi zaidi siku ya mwisho ya
kuhama wachezaji, ambapo jumla ya £210m zilitumiwa.
Licha ya klabu
za Ligi ya Premia kutumia £1.4bn kipindi chote cha kuhama wachezaji-
ambayo ni rekodi mpya - Alexis Sanchez, Virgil van Dijk, Riyad Mahrez,
Thomas Lemar, Diego Costa na Ross Barkley bado hawakufanikiwa kuhama.
Siku ya mwisho ya kuhama wachezaji msimu uliopita ilikuwa £155m.
Chelsea
walitumia £35m kumnunua Danny Drinkwater naye Mamadou Sakho
akanunuliwa £26m na Crystal Palace kutoka Liverpool, taarifa za kuhama
kwao zikitangazwa baada ya muda rasmi wa kuhama wachezaji.
Wawili hao ndio waliosaidia kuvunja rekodi ya mwaka jana.
Chelsea
walinunua pia Davide Zappacosta, Spurs wakamchukua mshambuliaji wa
Swansea Fernando Llorente kwa £15m, klabu hiyo ya Wales nayo ikajaza
nafasi hiyo kwa kumchukua Wilfried Bony kwa £12m.
Philippe
Coutinho, ambaye Barca waliwasilisha £114m mapema Agosti kutaka
kumchukua mapema Agosti lakini ombi lao likakataliwa, amesalia kuwa
mchezaji wa Liverpool lakini bado anaweza kuhama kwani dirisha la kuhama
wachezaji Uhispania litafungwa saa saba usiku Ijumaa.
Mahrez na Costa pia wamehusishwa na klabu za Uhispania.
Wachezaji waliothibitishwa kuhama awali Alhamisi walikuwa:
•Kylian Mbappe [Monaco - PSG] Mkopo, ambapo baadaye anaweza kununuliwa £165.7m
•Alex Oxlade-Chamberlain [Arsenal - Liverpool] £35m
•Serge Aurier [PSG - Tottenham] £23m
•Renato Sanches [Bayern Munich - Swansea] Mkopo
•Nikola Vlasic [Hajduk Split - Everton] £10m
Jumla
ya £1.4bn zilizotumiwa na klabu za Ligi ya Premia msimu huu zinazidi
rekodi ya msimu uliotangulia ya £1.120bn na ni karibu £1bn zaidi ya pesa
zilizotumiwa miaka mitano iliyopita.
Licha ya Manchester City kushindwa kumchukua Alexis Sanchez na beki
wa West Brom Jonny Evans, vijana hao wa Pep Guardiola ndio walioongoza
kwa kutumia £215m ambapo wanazidi klabu nyingine yoyote ile.
Paris
St-Germain walivunja rekodi kwa mchezaji binafsi kwa kumchukua Neymar
kwa £200m nao Barcelona wakamchukua Ousmane Dembele kwa £135.5m.
PSG
wameahidi kutoa £165.7m baadaye kumchukua Kylian Mbappe, ambaye kwa
sasa wamemchukua kwa mkopo, kwa mkataba wa kudumu majira ya joto mwaka
ujao.
Wachezaji ambao hawakuhama
Rekodi
iliyowekwa ingekuwa juu zaidi kwa £200m - iwapo baadhi ya wachezaji wa
thamani ya juu ambao walitarajiwa kuhama wangefanikiwa.
- Sanchez wa Arsenal alikaribia kuhamia kwa Manchester City kwa £55m. Lakini mkataba huo ulitegemea Lemar kujiunga na Gunners kujaza nafasi yake. Arsenal walikuwa wamekubaliana na Monaco kumchukua kwa £90m, uhamisho ambao ungemfanya wa tatu kwa thamani, lakini mchezaji huyo wa Ufaransa alikataa kuhama na hivyo Sanchez naye akakwama.
- Kiungo wa kati wa Everton Barkley, ambaye kwa sasa amejeruhiwa, alikataa kuhamia Chelsea kwa£30m - hata baada ya kudaiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu. Barkley amesalia na mwaka mmoja Everton na hatatia saini mkataba mpya.
- Beki wa Southampton Van Dijk amekuwa akifanya mazoezi ya timu ya vijana ya klabu hiyo tangu alipoanza kujaribu kulazimisha kuhamia Liverpool. Lakini hilo halikufanikiwa, hivyo atasalia St Mary's.
- Mshambuliaji wa Chelsea Costa anaaminika kuwa nchi yake ya kuzaliwa ya Brazil baada ya kuambia hayupo katika mipango ya meneja Antonio Conte. Lakini hakuhama. Hali isipobadilika, hataweza kucheza kwa kipindi cha hadi miezi minne.
- Winga wa Leicester Mahrez aliruhusiwa kusafiri Ulaya na timu ya taifa ya Ulaya kukamilisha uhamisho wake, lakini yamkini hakuna aliyefanya juhudi za kumsajili. Roma walikuwa wametaka kumnunua lakini dau zao zikakataliwa mara kadha awali.
- Manchester City waliacha kumtafuta beki wa West Brom Evans baada ya kushindwa kumuuza Eliaquim Mangala kwa Crystal Palace.
Wachezaji waliohama ambao huenda hukusikia
Mshambuliaji
wa timu ya taifa ya England ya vijana wa chini ya miaka 17 Jadon Sancho
alihamia Borussia Dortmund kutoka Manchester City kwa £10m, ambapo
alipewa jezi nambari saba ya Ousmane Dembele.
Chipukizi mwingine wa England alihamia Ujerumani, Liverpool walimkabidhi Ryan Kent kwa mkopo kwa Freiburg.
Liverpool pia walimkabidhi Divock Origi kwa Wolfsburg kwa mkopo.
Klabu ya Harry Redknapp Birmingham alivunja rekodi ya klabu hiyo kumnunua winga wa Brentford Jota kwa zaidi ya £6m.
Lazio walimchukua winga wa zamani wa Manchester United Nani kutoka Valencia kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Stoke City walimtuma Giannelli Imbula (Toulouse) na mshambuliaji Bojan Krkic (Alaves) kwa mkopo kwa msimu mmoja.
Arsenal
walimkabidhi Lucas Perez kwa Deportivo La Coruna kwa mkopo, mwaka mmoja
baada ya kulipa kiasi sawa kwa klabu hiyo £17.1m kumchukua.
Kiungo wa kati wa England Ravel Morrison aliondoka Lazio na kwenda klabu ya Atlas ya Mexico.
0 comments:
Post a Comment