KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Almasi ya Petra Diamonds imesimamisha shughuli zake za uchimbaji katika mgodi wake uliopo Mwadui Shinyanga, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Hii imekuja siku chache tu baada ya
kamati za bunge kuwasilisha ripoti zao kwa Rais John Magufuli kufuatia
uchunguzi walioufanya katika sekta ya uchimbaji madini ya almasi na
tanzanite.
Petra, ambao ndio wachimbaji wakubwa wa
Almasi nchini Tanzania, wamekuwa wamejikuta kuwa kampuni nyingine ya
kigeni kuingia katika mgogoro serikali ya Tanzania katika harakati za
kufanya mageuzi katika sekta ya uchimbaji madini nchini humo.
Wiki mbili zilizopita, mamlaka nchini
Tanzania ziliripoti kukamatwa kwa vifurushi vya almasi katika uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ambavyo vilikuwa ni mali ya Petra
na vilikuwa mbioni kusafirishwa kwenda Ubelgiji kuuzwa.
Maafisa wa serikali walisema Petra
ilidanganya juu ya kiasi na thamani ya almasi hizo ambapo, wakati
kampuni ya Petra ikisema almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola za
kimarekani milioni 14.8, uchunguzi wa serikali ulibaini almasi hiyo
ilikuwa na thamani ya dola milioni 29.5.
Hata hivyo, Petra imekanusha tuhuma
hizo na kusema kwanza wao ni wawazi katika kuripoti thamani ya almasi
yake lakini pia ni wakala wa serikali ndio unaokisia na kutoa thamani ya
almasi inayochimbwa na kampuni hiyo.
Mwandishi wetu Sammy Awami akiwa Dar es
Salaam anasema katika waraka wake leo hii, Petra imesema pia kwamba
baadhi ya maafisa wake wa ngazi za juu wanahojiwa na mamlaka nchini
Tanzania kuhusiana na sakata hiyo.
Kuhusu kufungwa kwa mgodi wake wa
Williamson uliopo Mwadui, Shinyanga, Petra imesema uamuzi huo wameufikia
kutokana na sababu za “kiafya na kiusalama” na kwamba wanaendelea kutoa
ushirikiano wao kwa serikali ya Tanzania katika uchunguzi wa mkasa
unaoendelea hivi sasa.
Serikali ya Tanzania imeendelea na
harakati zake za kimapinduzi katika sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya
mkakati wa Rais Magufuli kuona sekta hiyo inachangia zaidi katika pato
la taifa.
Tayari kuna sheria kali ambazo
zimewekwa kuhakikisha kwamba sekta ya madini nchini Tanzania inabanwa
katika kuchangia zaidi mapato kwa serikali.
0 comments:
Post a Comment