Erasto Nyoni alifunga goli lake la kwanza kwenye msimu mpya
wa ligi (2017/2018) huku akiwa na jezi ya Simba, kumbuka ilikuwa siku ya
ufunguzi wa ligi kuu Tanzania bara August 26, 2017 ambapo Ruvu Shooting
walinyanyasika kwa kufungwa bao 7-0.
Nyoni siku hiyo alicheza kama beki wa kushoto wa Simba, Nyoni ndio
alifunga goli la sita dakika ya 81. Baada ya kufunga goli hilo, Nyoni
alikwenda moja kwa moja kwenye bango lenye picha ya marehemu Patrick
Mafisango na kuionesha picha hiyo.
Mafisango aliwahi kuichezea Simba huku akitajwa kuwa miongoni mwa
wachezaji wa kigeni waliofanya vizuri katika klabu hiyo katika eneo la
kiungo. Mafisango alifariki May 17, 2012 kwa ajali ya gari.
moja ya vyombo vya habari hapa nchini kikaamua kumtafuta Nyoni
kutaka kujua ni kwa nini aliamua kwenda kushangilia kwenye picha ya
Mafisango? Alikuwa anamaanisha nini ili watu wengine wapate kujua.
“Kifo cha Mafisango kilinihuzunisha sana, jamaa alikuwa mtu safi sana
hakuna mtu ambaye amewahi kuniambia aliwahi kuwa na matatizo na
Mafisango tangu nimemfahamu,” Erasto Nyoni.
Urafiki wa Nyoni na Mafisango
“Unajua watu wengi hawajui kuwa mimi na Mafisango tulikuwa marafiki
sana kabla ya kukutana Azam FC, tulifahamiana wakati mimi nacheza
Burundi (Vital’O) yeye akiwa Rwanda. Tulikuwa tunakutana kwenye mechi za
kirafiki za vilabu vyetu huko ndio tulianza kuwa marafiki.”
“Baadae mimi nikarudi Tanzania nikajiunga na Azam, kama bahati
Mafisango akasajiliwa na Azam tukawa wachezaji wa timu mmoja. Urafiki
ukazidi kukua tukawa ndugu kabisa tunasaidia kwenye mambo yetu
mbalimbali. Hata alipoondoka Azam na kujiunga na Simba bado tuliendelea
kuwa karibu sana.”
Haikuwa bahati mbaya kwenda kwenda kwenye picha ya Mafisango, alijipanga
“Kabla mechi haijaanza nililiona bango la mashabiki likiwa na picha
ya maremu Mafisango, ghafla nikamkumbuka sana. Nikaomba Mungu kwamba
endapo ikitokea nikafunga goli kwenye ule mchezo basi nitaenda
kushangilia kwenye picha ya Mafisango. Bahati nzuri Mungu akafanikisha
nikafunga ndio maana niakenda kwenye picha ya Mafisango.”
Alikuwa anamaanisha nini kwenye picha ya Mafisango?
“Ni ishara ya kumuenzi na heshima kwake, hakuna mtu ambaye hajui kazi
ya Mafisango uwanjani kwa hiyo kwa upande wangu niliamua kwenda kutoa
heshima kwa rafiki yangu kipenzi.”
Klabu ya Simba imeamua kumuenzi marehemu Mafisango kwa kuistaafisha
jezi namba 30 ambayo ilikuwa ikivaliwa na Mafisango mchezaji wa kimatafa
wa Rwanda aliyezaliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
0 comments:
Post a Comment