Wednesday, 6 September 2017

BAADA YA NJOMBE KUIOMBA MSAMAHA YANGA LWANDAMINA AJIBU

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina.
KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, amesema kuwa, watakachowafanya Njombe Mji, itakuwa salamu kwa timu nyingine kwamba ndiyo wameanza kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara.

Yanga ambayo ndiyo bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Jumapili ijayo itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe kucheza dhidi ya wenyeji wao, Njombe Mji ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Lwandamina ambaye ni raia wa Zambia, amesema baada ya kuanza msimu kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli na kuonekana kama hawawezi kutetea taji lao, sasa wamedhamiria kushinda mechi ijayo kwa kishindo ili kuthibitisha ubora wao.

Mzambia huyo ambaye hivi karibuni aliiacha Yanga na kwenda kwao kushughulikia masuala ya mazishi ya baba yake, amesema: “Nimerejea tayari na moja kwa moja nimeanza kazi ya kuwanoa vijana wangu tukijiandaa na mechi yetu ijayo ya ligi tutakayocheza ugenini.

“Najua msimu huu kila timu imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri, hivyo basi baada ya kuona tumetoka sare mechi ya kwanza, tunajipanga kushinda mechi ijayo ili kudhihirisha ubora wetu ambao tuliokuwa nao msimu uliopita mpaka tukawa mabingwa.
“Tunataka kutetea taji letu na safari ya kufanya hivyo tunaianzia Njombe, baada ya hapo mambo yote nadhani yatakaa sawa, tunataka kushinda kila mechi iliyo mbele yetu ili kutetea taji letu.”
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive