Thursday 31 August 2017

WENYE VYETI FEKI WAOMBEWA SERIKALINI


SHIRIKISHO la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (Tucta), limeiomba Serikali kuangalia upya hatua ya kuwatoa katika ajira watumishi waliogundulika kuwa na vyeti feki, ili kuwalipa kifuta jasho kutokana na kulitumikia Taifa kwa miaka mingi.


Aidha Tucta imesema inajua watu hao walifanya makosa, lakini serikali inapaswa kuwasaidia, ili kupunguza umaskini mbeleni kutokana na wengine umri wa kustaafu ulikuwa umekaribia.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Yahya Msigwa, katika warsha ya kupitia upya sera za Ukimwi na Afya kwa watumishi iliyowahusisha wataalamu kutoka vyama vya wafanyakazi.

Msigwa alisema kuwatoa katika ajira bila kuwapa chochote kunawafanya watumishi hao kuwa maskini ghafla, kwani maisha ya mtumishi ni mshahara wake na haki yake kazini.

Msigwa alisema Tucta haina tatizo na uamuzi huo wa serikali, lakini watumishi wengine wana mikopo katika taasisi za fedha na benki.

"Kuwatoa ghafla watumishi hao hata benki zinaathirika kwani mikopo hairejeshwi, hivyo suala hilo liangaliwe upya kwa sababu hata benki zinaweza kufa kwa kutorejeshewa fedha zao,” alisema Msigwa.

Alisema ingawa ni makosa kisheria kwa mtumishi kuwa na cheti feki, lakini iangalie kwa jicho la karibu kuwa watumishi hao wana wategemezi ambao walikuwa wakitegemea mishahara ya ndugu zao.

“Sisi kama Tucta hatuna ugomvi na serikali, lakini ombi letu serikali iangalie jinsi ya kuwasaidia watumishi hawa hata kuwalipa fedha kidogo kwani walikuwa watumishi wazuri tu, ukiacha kosa walilokutwa nalo,” alisema Msigwa.

Alisema tatizo siyo wao bali ni mfumo uliokuwapo wakati wakiingia katika ajira zao kipindi cha nyuma, jambo ambalo nalo linapaswa kuangaliwa, ili waweze kunufaika kidogo.

Aliwataka viongozi wanaoshughulikia matatizo ya wafanyakazi kutatua changamoto zao haraka katika kipindi kifupi, ili kundoa kero ya kusubiri kwa muda mrefu kutatuliwa matatizo yao.

Alisema kumekuwapo na matatizo mengi ya wafanyakazi ambayo huchukua muda mrefu kutatuliwa, jambo ambalo linawakatisha tamaa.

Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Getrude Sima, alisema wako pamoja na vyama vya wafanyakazi

kuhakikisha sera wanayoipitisha inazingatiwa kwa weledi mkubwa na kuwataka washiriki katika upitiaji wa sera hizo kuzingatia jinsia.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive