Mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi.
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi amefunguka kuwa
kitendo cha timu yao kukamilika kila idara huku ikiwa na wachezaji wengi
wenye uwezo kama Haruna Niyonzima, hawana wasiwasi wakikutana na timu
yoyote ile hata iwe Yanga watamaliza mchezo mapema.
Okwi ambaye amesajiliwa klabuni hapo hivi karibuni, amesema kuwa
watakachokifanya katika kila mchezo ni kufunga mabao kadiri wawezavyo
kutokana na Niyonzima kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho.
Simba kwa sasa ipo kisiwani hapa ikiwa katika kambi ya maandalizi yake
kuelekea katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa
Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Okwi alisema kuwa uwepo wa mchezaji
huyo ndani ya timu yao ni faraja kubwa kwa kuwa ana uwezo wa kupiga pasi
za mwisho nzuri ambazo zitawafanya wafunge mabao ya kutosha msimu huu.
Haruna Niyonzima.
“Kwangu ni kitu cha faraja kucheza timu moja na mchezaji kama
Niyonzima kwa sababu kwanza anajua halafu ana uwezo mkubwa wa kupiga
pasi za mwisho kitu ambacho naamini kitatuongezea uwezo wa kufunga mabao
mengi msimu huu. “Naamini wapinzani tukikutana nao tutawafunga mapema
tu kutokana na kikosi chetu kukamilika kila idara kwa maana kwamba kila
mmoja wetu anatimiza majukumu yake ipasavyo,” alisema Okwi.
Wakati huohuo, Kocha wa Simba, Joseph Omog amebadilisha mbinu za
wachezaji wake na sasa wamekuwa wakifanya mazoezi ya kufunga kutoka
umbali wa mita 20. Katika mazoezi ya jana yaliyofanyika kwenye Uwanja wa
Ngome uliopo Fuoni, Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja walitoa
maelekezo kwa beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’
na kiraka Ally Shomary kupiga mipira ya krosi za juu wakitokea pembeni.
Kisha waliwapanga wachezaji wote kutoka nusu ya uwanja kwa umbali wa
mita 20 wakiwa na mipira ambayo waliwataka wapige mashuti golini
kulipokuwa na makipa watatu waliokuwa wakibadilisha kudaka ambao ni
Aishi Manula, Said Mohamed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja. Baadaye
walisogezwa hadi katika mstari wa eneo la 18 na kutakiwa kupiga mashuti
makali, walitekeleza hilo kwa ustadi.
source: Champion
0 comments:
Post a Comment