Tuesday, 8 August 2017

NIYONZIMA MAMBO MUBASHARA MSIMBAZI



Image result for niyonzima simba


HARUNA Niyonzima alizoeleka zaidi kuonekana kwenye uzi wa njano, lakini kuanzia leo Jumanne ni rasmi kwamba atakuwa Kisimba zaidi ndani ya uzi mwekundu.
Ni ngumu kumeza kwa mashabiki wa Yanga, lakini ndiyo ukweli. Niyonzima alifanya mazoezi na wenzake jana Jumatatu katika Uwanja wa Bunju, Dar es Salaam na leo atacheza mechi ya Simba Day dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, kitu kinachowafanya Wana Msimbazi kuchonga na kujiandaa kupokea burudani la kufa mtu kutoka kwa staa huyo.
Frank Kasanga ‘Bwalya’ ni beki wa zamani wa Simba, amemkaribisha Niyonzima ndani ya kikosi hicho na kusisitiza kwamba walimsubiria kwa muda mrefu: “Ni mchezaji mwenye uwezo wa juu na pengo lake Yanga litaonekana hata kama kwa sasa wanamponda.”
Bwalya alisema kitendo cha Yanga kumsajili Ibrahim Ajibu, kiliwaumiza mashabiki wa Simba na kudai ni zamu kwa zamu kwani kumpata Niyonzima, kumefuta machungu yao, wakiamini atakuwa msaada katika ligi na michuano ya kimataifa.
“Kilichobakia tunasubiri uhondo, unajua kuna raha ya watani wa jadi, walipomsajili Ajibu, tulikuwa hatunywi maji, kila tulipopita zilikuwa kejeli, wao kumkosa Niyonzima mara waseme mzee, sasa mbona wana Nadir Haroub ‘Cannaro’ na Thaban Kamusoko ambao umri wao, umeenda,” alisema.
Mwanamuziki wa kizazi kipya, 20 Percent alisema: “Niyonzima apige kazi, amefika Simba, aifanyie kitu ambacho kitamjengea heshima kwa maana kama ametoka Yanga, walikofanikiwa kutwaa ubingwa mara tatu ndivyo anatakiwa kufanya Simba, ili aendelee kuwa shujaa.”
Edibily Lunyamila, straika wa zamani wa Yanga, alisema: “Yanga, bado walikuwa wanauhitaji uwezo na huduma yake, ila walishindwana kwenye masilahi, akifanya vizuri atawafunga mdomo, ila akicheza chini ya uwezo basi anaweza kujikuta heshima yake ikishuka.”
Mwanamuziki wa kizazi kipya, Ruta Bushoke, alisema: “Ni kweli Niyonzima ni mchezaji mwenye kiwango, ila ni nafasi kwa wale wanaocheza safu yake kuonyesha uwezo wa kuziba pengo lake, pia ni fundisho kwa benchi la ufundi kutomtegemea mtu mmoja, kwa Simba Day naomba asifunge maana akifunga tu, atatunyima raha, pasi atoe tu, lakini si kufunga.”
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive