Friday 4 August 2017

MAYAI YENYE SUMU YATIA WASIWASI UJERUMANI

Onstwedde, Uholanzi 03 August 2017Haki miliki ya picha
Wasimamizi wa maduka ya jumla ya Aldi wameondoa mayai yote yaliyokuwa yanauzwa katika maduka hayo nchini Ujerumani baada ya kuibuka kwa wasiwasi kwamba huenda yana sumu.
Uchunguzi ulionesha kwamba kemikali aina ya fipronil, ambayo inaweza kudhuru figo, ini na tezi za shingoni za mwanadamu, ilikuwepo katika baadhi ya mayao yaliyokuwa yakiuzwa katika maduka hayo Uholanzi.
Fipronil hutumiwa kuua viroboto na kupe kwenye kuku.
Afisa mmoja nchini Ujerumani amesema mayai zaidi ya 10 milioni ambayo inaaminika huenda yana sumu yameuzwa nchini Ujerumani.
Waziri wa kilimo wa eneo la Lower Saxony Christian Meyer ameambia runinga moja ya Ujerumani kwamba kuna hatari kubwa hasa kwa watoto iwapo watakula zaidi ya mayai mawili kwa siku.
Mashamba 180 ya kufugia kuku nchini Uholanzi yamefungwa kwa muda siku za karibuni huku uchunguzi ukiendelea.
Afisa mwendesha mashtaka nchini Uholanzi Marieke van der Molen amesema uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha sumu hiyo.
Hayo yakijiri, maduka ya jumla barani Ulaya yamesitisha uuzaji wa mayai kutoka kwa vifurushi vya mayai ambavyo huenda viliambukizwa sumu hiyo.
Hata hivyo, Aldi, ambao wana karibu maduka 4,000 nchini Ujerumani, ndio wa kwanza kusitisha uuzaji wa mayai kama tahadhari.
Uholanzi ndiyo muuzaji nje mkubwa zaidi wa mayai na bidhaa za mayai Ulaya, na miongoni mwa muuzaji mkubwa duniani.
Inakadiriwa kwamba taifa hilo huzalisha zaidi ya mayai bilioni 10 kila mwaka, na asilimia 65 kati ya hayo huuzwa nje ya nchi hiyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive