Rais John Magufuli, amesema ifike wakati wizi uliokuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi wa
serikali wakishirikiana na wawekezaji kutoka nje ukomeshwe ili kuleta
maendeleo ya Tanzania kwa ajili ya wananchi wote na si watu wachache kujinufaisha.
Hayo ameyasema leo wakati akiwahutubia
wanachi wa Hale wilayani Korogwe wakati akianza ziara yake ya siku tano
mkoani Tanga ambapo atashirikiana na Rais Museveni wa Uganda kuweka jiwe
la msingi kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani kwenye mwambao wa bahari ya Tanga, Agosti 5 mwaka huu.
“Mlinipa kura nyingi sana na
ninawashukuru na ahadi yangu iko palepale kwamba sitawaangusha,
unapokuwa na kiongozi anayewatumikia wananchi ni jambo nzuri.
“Hatukuumbwa kwa ajili ya kuwa
wasindikizaji wa watu bali tumeumbwa ili kuwa Tanzania yenye neema ndiyo
maana hata kwenye kutumbua majipu huwa sijali hata kama ni Mzungu. Wapo
Wazungu waliokuwa wamezoea kutumbua dhahabu yetu, nimeamua kuwatumbua
bila aibu ili kutengeneza rasilimali za Watanzania kwani mwizi ni mwizi tu, awe Mzungu, awe wa CCM, awe wa Chadema, awe wa CUF au hata kama hana chama.
“Nitasimama kwa ajili ya Watanzania wanyonge bila kujali itikadi zenu kwa sababu lengo langu mimi ni kuleta maendeleo,” alisema Rais Magufuli.
Aidha rais ameeleza kuwa kwa Afrika
mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya
Tanga ni mradi mkubwa ambapo amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo
kupata maendeleo kwani watu zaidi ya 18,000 watapata ajira.
0 comments:
Post a Comment