Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (Chadema).
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (Chadema)
amesema kuwa baadhi ya madiwani waliojiuzulu na kukihama chama hicho
hivi karibuni wamekiandikia chama hicho barua wakiomba kurejea.
Meya huyo wa Ubungo ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na
kipindi cha Maisha Mseto cha 100.5 Times FM, ambapo ameeleza kuwa
madiwani hao walirubuniwa kwa ahadi ya fedha ambayo hata hivyo
haikutekelezwa kama walivyokubaliana baada ya kujiuzulu.
“Baadhi ya madiwani wametuandikia barua wanaomba kurudi, wanadhani
labda wakirudi watarudi kwenye nafasi zao za udiwani kwa sababu ahadi
walizokuwa wamepewa za fedha hazikutimizwa,” alisema Jacob.
Kiongozi huyo wa Chadema alidai kuwa kinachofanyika hivi sasa ni
siasa za kununua wanachama kama ilivyo kwa vilabu vya soka kununua
wachezaji kutoka katika vilabu pinzani.
Alipotakiwa kutoa ushahidi unaoonesha kuwa madiwani hao walipewa
fedha na kiasi gani, alisema kuwa wakati wa kufanya mazungumzo walikuwa
wanaitwa madiwani kadhaa na watu ambao alidai ni wa chama fulani, lakini
baada ya mazungumzo wapo waliokataa mpango huo na kwamba ndiyo walitoa
siri za majadiliano hayo.
“Sio kiasi kikubwa cha fedha, wengine waliahidiwa shilingi milioni 10
lakini baada ya kujiuzulu walipewa shilingi milioni tatu. Kuna mwingine
aliadiwa shilingi milioni tatu na zikawekwa benki kabisa, lakini baada
ya kujiuzulu fedha hizo ziliondolewa kwenye akaunti yake na benki
ikamueleza kuwa aliyeweka ameieleza benki hiyo kuwa aliweka kimakosa
hivyo alirejeshewa,” Jacob alidai.
Hata hivyo, alidai kuwa madiwani wa Dar es Salaam ‘hawajanunuliwa’
kwani wengi wanajitambua, wanamsimamo zaidi na wana uwezo wa kifedha
angalau usiowafanya kurubuniwa kirahisi.
Jacob alisema kuwa kurejea uchaguzi kwenye kata ambazo madiwani hao
wamejiuzulu kutaisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni
kugharamia uchaguzi huku akitamba kuwa Chadema itarejesha nafasi hizo.
Zaidi ya madiwani kumi walijiuzulu nafasi zao miezi michache
iliyopita na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi wakieleza kuwa
hawakushinikizwa na mtu yeyote bali wameridhishwa na utendaji wa Rais
John Magufuli.
0 comments:
Post a Comment