Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki moja.
Bulaya alikimbizwa Muhimbili kutoka tarime mkoani Mara baada ya kupata tatizo la kupumua baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya kituo cha polisi mjini Tarime. Alikuwa amelazwa wodi namba 18 katika jengo la Sewahaji akipatiwa matibabu.
Mbunge huyo wa Chadema, jana Agosti 28 ameruhusiwa kutoka hospitali na amewashukuru madaktari wa Muhimbili kwa kumpatia matibabu ya kina.
Amesema afya yake imetengemaa lakini amepewa maelekezo kadhaa.
“Kwanza nitapumzika kwa siku 10, hivyo ndivyo nilivyoagizwa na nitatakiwa kurudi tena hospitalini kwa ajili ya kuangaliwa afya yangu zaidi. Kwa sasa nitapumzika kabla ya kurudi jimboni kuendelea na shughuli za maendeleo,” amesema Bulaya.
Bulaya aliwekwa rumande Agosti 18 baada ya kukamatwa na polisi akidaiwa kuingia jimbo la Tarime kufanya shughuli za kisiasa kwa kutoa msaada wa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi kwa mwaliko wa mbunge mwenzake Esther Matiko.
0 comments:
Post a Comment