SIMBA
imeianza Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kishindo baada ya kuifumua Ruvu
Shooting mabao 7-0 na kuiacha timu hiyo kileleni, lakini kama unadhani
Simba wameridhika na ushindi huo pole, kwani Kocha Mkuu wake, Joseph
Omog, amesema utamu zaidi unakuja.
Mcameroon huyo
amesema ushindi huo ni ishara tosha kuwa mambo mazuri yanakuja katika
timu yao, hivyo mashabiki wakae mkao wa kula na waache kulaumu wachezaji
wao.
Omog alisema kwanza mechi hiyo imeingia katika
historia yake ya soka tangu alipojiunga na kikosi cha Simba Julai 2016,
kwani hakuwahi kupata ushindi mkubwa kama huo.
“Washambuliaji
wangu wameanza kupokea vema maelekezo niliyokuwa nawapa tangu tukiwa
kambini Afrika Kusini, naamini moto utawaka zaidi kadiri ligi
itakavyosonga mbele,” alisema.
“Mashabiki na wapenzi wa
Simba wanatakiwa watulie na kuacha kuwalaumu wachezaji, kwani siku
zinavyozidi kwenda watafurahi kila mechi.”
BOCCO
AISUBIRI AZAM
Katika
hatua nyingine, straika John Bocco ‘Adebayor’ amesajiliwa na Simba
kutoka Azam na kuzikosa mechi za Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na ya
ufunguzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting.
Hata
hivyo taarifa nzuri ni kwamba mchezaji huyo aliyekuwa akisumbuliwa na
maumivu ya nyama za paja, sasa anaweza kuvaana na timu yake ya zamani
wakati timu hizo zitakapopambana wiki ijayo.
Daktari wa
Simba, Yassin Gembe, amesema Bocco anaendelea vizuri, lakini aliamua
kumpumzisha katika mechi ya Ruvu Shooting ili kuweza kuimarika zaidi.
“Bocco
anaendelea vizuri lakini kwa usalama zaidi nimemuongezea mazoezi
binafsi ya peke yake ili kuweza kuwa fiti zaidi na mechi ambayo itakuwa
ya kwanza kwake kimashindano akiwa na Simba itakuwa dhidi ya timu yake
za zamani Azam,” alisema Dk Gembe.
0 comments:
Post a Comment