Edward Lowassa.
Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema licha ya changamoto nyingi
anazopata akiwa ndani ya upinzani, atagombea tena urais katika Uchaguzi
Mkuu mwaka 2020 na anaamini atashinda.
Lowassa aliyejitokeza kugombea urais
kupitia CCM mwaka 2015 na jina lake kukatwa kisha kuhamia Chadema
alikogombea nafasi hiyo akiwakilisha vyama vilivyoungana chini ya Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kushindwa na Rais John Magufuli, bado
anatajwa kuwa mgombea mwenye nguvu katika kambi ya upinzani.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), Rais Magufuli alishinda kwa kupata kura 8,882,935 sawa
na asilimia 58.46, huku Lowassa wa Chadema akijipatia kura 6,072,848
sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Akizungumza jana katika mahojiano
maalumu na waandishi wa Nation Media Group (NMG) jijini Nairobi, Lowassa
alisema, “Kwa mapenzi ya Mungu nitajaribu tena mwaka 2020 na nitapita
kwa mikono safi.”
Kama ambavyo amekuwa akisema tangu
aliposhindwa katika uchaguzi huo wa 2015, pia jana Lowassa alisema licha
ya kuendeshwa katika mfumo usioaminika, hakutaka kuwashawishi wafuasi
wake wamwage damu kwa kudai ushindi.
“Wafuasi wangu walitaka tuingie
mitaani kudai ushindi, lakini kulikuwa na bunduki nyingi mikononi mwa
wanajeshi. Niliogopeshwa na umwagikaji wa damu. Sikutaka kuingia Ikulu
kupitia damu za watu kwa sababu sistahili hivyo,” alisema.
Hata hivyo, alisema licha ya uchaguzi
huo kutoaminika, bado anamheshimu Dk Magufuli kama Rais, japo mbunge
huyo wa zamani wa Monduli alikataa kukubaliana na utendaji wa mkuu huyo
wa nchi kwa kipindi alichokaa madarakani.
“Hata kama Dk Magufuli
alichaguliwa katika mfumo usioaminika wa uchaguzi, bado tunamheshimu
kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Lowassa.
Alisema, “Utendaji wa Rais
Magufuli utaamuliwa na watu utakapofika mwisho wa muhula huu mwaka 2020.
Bora niwe makini katika hili nisije nikanukuliwa vibaya nikaingia
kwenye matatizo nitakaporudi nyumbani.”
Lowassa ambaye hivi karibuni amekuwa
akiripoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kutokana
na kauli yake kuhusu viongozi wa Jumuiya ya Uamsho waliokamatwa mwaka
2012 huko Zanzibar, alilaani ukiukwaji wa demokrasia akisema Chadema
itakwenda mahakamani kudai haki ya kufanya siasa.
“Kukataza huko siasa ni kinyume
cha demokrasia na haki, hata hivyo tunajitahidi kujiimarisha.
Tumeshalalamika serikalini kuondoa katazo hilo lakini bado inajivuta
miguu. Tunaweza kulazimika kwenda kutafuta msaada wa Mahakama,” alisema.
Kuhusu kamatakamata ya viongozi wa
upinzani, Lowassa alisema licha ya kupata zaidi ya kura milioni sita,
ameshindwa hata kuwashukuru wananchi waliompigia kura.
“Nilipata kura milioni sita na
siwezi kufanya mikutano hata ya kuwashukuru watu kwa kunipigia kura.
Hiyo si tu kinyume cha demokrasia, bali si haki,” alisema Lowassa.
Wakati Jeshi la Polisi likikataza
vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara mwaka 2016, Rais Magufuli
alisema wanasiasa waliochaguliwa wanaweza kufanya mikutano kwenye
majimbo yao.
Hata hivyo, bado baadhi ya mikutano ya ndani ya vyama hivyo imeendelea kuzuiwa na viongozi wa upinzani wakikamatwa.
Licha ya kukiri kuwa ndani ya
upinzani kuna changamoto nyingi, Lowassa alisema kuna wakati anapata
faraja kuwa upande huo wa siasa.
“Ni uzoefu mzuri unaoendana na
nyakati nzuri na ninafurahia uzoefu huo kwa sababu mimi bado ni maarufu
na nina wafuasi wengi. Kukataza shughuli za siasa ni hatua ya
kuninyamazisha,” alisema.
Lowassa alisisitiza msimamo wa
Chadema wa kumuunga mkono Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 8 akisema kiongozi huyo ni chaguo
sahihi kwa demokrasia za Kenya.
“Tumekuwa na vikao halali kama
chama na vya wazi na kukubaliana kumuunga mkono Uhuru Kenyatta
achaguliwe tena. Ni mtu mzuri anayeunga mkono Jumuiya ya Afrika
Mashariki na anaheshimu viongozi wa upinzani,” alisema.
Hata hivyo, Lowassa aliyekwenda Kenya
kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Usalama, Jenerali Joseph
Nkaisery alifafanua kuwa uamuzi wa kiongozi sahihi wa kuiongoza Kenya
utafanywa na Wakenya wenyewe kwenye uchaguzi wa Agosti.
Alipoulizwa ni kwa nini Chadema
imebadilisha mgombea wanayemuunga mkono katika uchaguzi wa Kenya, kutoka
kwa Raila Odinga wa Nasa, Lowassa alisema amekuwa akimuunga mkono
Kenyatta kwa muda mrefu.
Kabla Lowassa hajajiunga na Chadema,
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alishatangaza kumuunga mkono
Odinga wakati huo akiwa Waziri Mkuu wa Kenya.
Akizungumzia kauli ya Lowassa
kumuunga mkono Kenyatta, mmoja wa viongozi wa muungano wa Nasa, Musalia
Mudavadi alimtaka kiongozi huyo aache kuwaingilia katika uchaguzi huo
na badala yake apambane na Dk Magufuli Tanzania.
CREDIT: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment