Wednesday, 12 July 2017

NGELEJA AFUNGUKA NI KWANINI HAJAMRUDISHIA FEDHA RUGEMALIRA



Image result for ngeleja

Mtumiaji wa moja ya mitandao wa kijamii, jana alituma kituko katika ukurasa wake akiwataka wote aliowapa fedha wamrejeshee iwapo hawazitaki badala ya kuzipeleka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akisema anapatikana wakati wote.



Alikuwa akidhihaki kitendo cha Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kupeleka TRA Sh40.4 milioni badala ya kuzirejesha kwa mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira aliyempa fedha hizo.

Kitendo hicho kilitawala mijadala katika mitandao ya kijamii, lakini Ngeleja aliamua kutoa ufafanuzi zaidi wa sababu zilizomfanya asirejeshe fedha hizo kwa Rugemalira baada ya maelezo ya juzi kutotosheleza.

Fedha alizopewa ni sehemu ya Sh306 bilioni zilizochotwa kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow mwaka 2014 na kusababisha mjadala mkubwa bungeni uliosababisha kujiuzulu kwa mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wenyeviti wa kamati za Bunge kuvuliwa madaraka na baadhi ya watumishi wa umma kufikishwa mahakamani.

Baada ya takriban miaka mitatu, Ngeleja, ambaye alivuliwa uenyekiti wa kamati ya Bunge kutokana na maazimio ya Bunge, juzi alitangaza kurejesha fedha hizo serikalini kupitia TRA, akisema kitendo cha Serikali kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wawili wakuu katika sakata hilo, kinaonyesha kuna harufu ya rushwa.

Lakini maswali mengi yaliibuka, likiwamo la sababu za kuzipeleka fedha hizo TRA badala ya Hazina au kumrudishia aliyempa, lakini mbunge huyo ametoa maelezo zaidi.

“Kwa mazingira halisi yanayomkabili aliyenipa msaada (Rugenalira), mahali salama pa kurejesha hizo fedha sasa ni serikalini,” amesema Ngeleja katika ujumbe mfupi alioutuma kwa gazeti hili.

“Serikali itajua kuwa fedha hizo zinastahili kwenda kwa Rugemalira sasa au wasubiri hatima ya kesi.

“Ningezirudisha kwa Ruge, watu wangeweza kuibua hoja kwamba labda napiga changa la macho tu.”

Kwa kurejesha fedha hizo, Ngeleja sasa anakuwa amelipa jumla ya Sh53.57 milioni, kwa kujumlisha na kodi aliyolipa awali.

Rugemalira, ambaye kampuni yake ya VIP Engineering ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL, na Harbinder Singh Seth, ambaye ni mwenyekiti mtendaji wa Pan African Power Solution (PAP) inayomiliki kampuni hiyo, kwa sasa wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kuhujumu uchumi na kutakatisha fedha.

Fedha hizo zilikuwa zinakusanywa kwenye akaunti hiyo baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni inayofua umeme ya IPTL kuingia katika mgogoro kuhusu kiwango cha tozo ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa taratibu za akaunti kama hizo, fedha hutakiwa kutolewa kwa ridhaa za pande zote mbili na kesi inapoisha, pande hizo hukutana kukokotoa stahiki za kila upande.

Lakini zilichotwa na baadaye kuonekana zikiingia katika akaunti za mawaziri, majaji, viongozi wa dini, watumishi waandamizi wa umma na wabunge, akiwamo Ngeleja.

Juzi, Ngeleja, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini alisema amepitishia fedha hizo TRA kwa kuwa Serikali ni moja na jana alisisitiza msimamo wake.

Mazungumzo kati ya Mwananchi na Ngeleja jana yalikuwa hivi;

Swali: Kwa nini umerudisha sasa na si siku za nyuma kwani sakata hili limeibuka karibu miaka mitatu iliyopita?

Ngeleja: Hata aliyenipa msaada Serikali ilikuwa haijamchukulia hatua kama ilizomchukulia sasa. Nilidhani msaada ule haukuwa na matatizo ukizingatia kodi tayari nilishaulipia asilimia 30.

Kitendo cha mbunge huyo kurudisha fedha kimelinganishwa na msamaha alioutoa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa watu waliochota fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kuwa wasingefikishwa mahakamani kama wangerejesha. Hata hivyo, Rais John Magufuli hajatangaza msamaha kama huo, badala yake Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Valentino Mlowola aliiambia Mwananchi katika mahojiano mwaka jana kuwa yeyote aliyeingiziwa fedha hizo, asidhani amepona.

Wengine walioingiziwa fedha hizo ni Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi (Sh1.6 bilioni) sawa na Andrew Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi, CCM), na Paul Kimiti (Sh40.4 milioni).

Wengine ni Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Dk Enos Bukuku (aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco Sh161.7 milioni), Jaji John Ruhangisa (Sh404.25 milioni), Jaji Aloysis Mujilizi (Sh40.4 milioni), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni), na Emmanuel ole Naiko (mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Uwekezaj, Sh40.4 milioni).

Pia yupo ofisa wa TRA Lucy Appolo (Sh80.9 milioni), Askofu Msaidizi Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Msaidizi Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).

Akitoa maoni yake kuhusu hatua ya Ngeleja, David Kafulila, mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini aliyeibua sakata hilo bungeni, alisema uamuzi huo hauna tofauti na alichofanya Rais mstaafu Kikwete katika sakata la EPA, ambao ulikuwa kinyume cha sheria kwa kuwa jinai haifutwi kwa kurejesha kilichoporwa.

“Uamuzi wa Ngeleja ni hatua ya kwanza kwamba amekubali jinai na amerudisha na hivyo wenzake pia wazirudishe ili wabaki na jinai ya ‘kwa nini walijipatia fedha hizo isivyo halali’. Kifupi kurudisha fedha hizo hakumwondolei jinai yeyote aliyehusika,” ameandika Kafulila katika ukurasa wake wa Facebook.     
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive