Wednesday 12 July 2017

LISSU-NGELEJA NA WENZAKE WAKAMATWE HARAKA


Image result for lissu

SIKU moja baada ya William Ngeleja kutangaza kurejesha serikalini fedha zinazodaiwa zao la kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu,amesema Mbunge huyo wa Sengerema (CCM) na watu wote waliopata mgawo huo wanatakiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa kuwa ameuthibitishia umma kuwa ni mla rushwa.


Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali iliyopita, juzi alizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) na kutangaza kuwa ameamua kurejesha Sh. milioni 40.4 alizopewa na Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engineering na mmiliki mwenza kwa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.

Mkurugenzi huyo na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP), Habinder Sethi Sigh, wako mahabusu kwenye Gereza la Keko, Dar es Salaam, baada ya kukosa dhamana walipofikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wiki mbili zilizopita na kusomewa mashtaka 12, yakiwamo ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4.

Akizungumza jana na Nipashe kwa simu jana, Lissu alisema sasa hakuna ubishi kuwa Ngeleja alitumia madaraka vibaya kujipatia fedha hizo na kuwa sehemu ya mafisadi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi, Ngeleja ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, alisema amefikia uamuzi huo wa kuzikabidhi Sh. milioni 40.4 katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA) ili kujiweka kando na kashfa kwa kuwa aliyempa ni mtuhumiwa.

Lissu alidai maelezo ya Ngeleja yanadhihirisha kuwa ni mla rushwa na mwongo kutokana na sababu yake kwamba aliyempa ameingia kwenye kashfa, kwa kuwa sakata hilo si jipya, liliibuka Novemba 2014 na aliondolewa kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge.

"Kusema alijua juzi kuwa fedha hizi zinahusishwa na kashfa ni kutudanganya. Anatakiwa kukamatwa," Lissu alisema.

"Nchi hii ukiiba ukakamatwa umeiba ndiyo kesi imeisha? "Sheria ni kuwa umeiba, umekamatwa unafikishwa kwenye vyombo vya dola ukikutwa na hatia unafungwa na fedha unarudisha."

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Singida Mashariki, alisema uamuzi wa mbunge mwenzake huyo kupeleka fedha za kashfa TRA unazua maswali zaidi kwa kuwa alipewa na Rugemalira na viongozi wa awamu iliyopita walisema si za umma bali mtu binafsi.

"Ngeleja anatuambia kuwa alizilipia kodi, kwa hiyo ukiiba na ukazilipia kodi dhambi inaisha?" Lissu alihoji ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzanui Bungeni/ "Alirudisha TRA kwani alipewa na TRA? Fedha za mtu binafsi zinawezaje kurejeshwa TRA?

Kwa nini zisirejeshwe benki (akaunti ya Rugemalira)? "Nitamshangaa Rais asipochukua hatua dhidi ya mtu huyo ambaye amekiri moja kwa moja." Lissu pia alikumbusha: "Wakati tunawafukuza bungeni mwaka 2014, tulisema wanatakiwa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria -- wakamatwe, wafunguliwe mashtaka, wakipatikana na hatia wafungwe."

Alisema bila kujali vyeo na nafasi zao kwenye jamii, wote walionufaika na mgawo wa fedha hizo wanapaswa kuwajibika kwa kuwa hata unapokuwa kiongozi wa dini hupaswi kula rushwa au kuchukua fedha za rushwa.

Alisema yako maswali magumu kwenye suala la akaunti ya Tegeta Escrow likiwamo la aliyeruhusu fedha zitoke kwenye akaunti iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika kikao cha 18 cha Bunge la 10, ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilianika orodha ya waliopata mgawo wakiwamo aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge, ambao kila mmoja alipata Sh. bilioni 1.6.

Prof. Tibaijuka alipigiwa simu na Nipashe jana saa 10:25 alasiri, lakini akakata simu baada ya mwandishi kumuuliza kama atafuata nyayo za Ngeleja kurejesha kiasi cha fedha alichopewa.

Nipashe pia ilimtafuta Chenge kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake haikupokelewa. Wengine ni aliyekuwa Mnikulu wakati wa uongozi wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, Shaaban Gurumo, aliyepewa Sh. milioni 80, Jaji wa Mahakama Kuu, Eudes Ruhangisa alipata Sh. milioni 404.25 na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Dk. Enos Bukuku, aliyepewa Sh. milioni 161.7.

Katika ripoti hiyo Waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, Mbunge wa zamani wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko, na Jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Aloisius Mujulizi walitajwa kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.

Wengine ni ofisa wa TRA, Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Rita), Philip Saliboko Sh. milioni 40.2, maaskofu Methodius Kilaini Sh. milioni 80.9 na Eusebius Nzingirwa Sh. milioni 40.4, Padri Alphonce Twimannye Sh. milioni 40.4, maofisa wa Rita Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na Theophil Rugozobwa Sh. milioni 323.4.

Lissu alisema ndani ya siku moja zilitoka Sh. bilioni 78 na ziligawanywa kwa viongozi wa dini, watumishi wa umma na wabunge.

Aidha, nguli huyo wa sheria alidai aliyeandika kijikaratasi fedha hizo zitoke BoT ni aliyekuwa msaidizi wa Rais, Prosper Mbena, ambaye haelezi alipokea maelekezo kutoka kwa nani. Mbena kwa sasa ni Mbunge wa Morogoro Kusini (CCM).

Alisema wako watu ambao hawajitengi mbali na mkono wa sheria kutokana na kashfa hiyo akiwamo Gavana wa BoT, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali.

Lissu pia alisema hadi sasa haijulikani kiasi cha Sh. bilioni 73 zilizoingizwa kwenye akaunti ya Stanbic zilichukuliwa na nani na zilipelekwa wapi.

Kauli ya Lissu imeungwa mkono na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi), ambaye jana alisema: "Kurudisha fedha hizo hakumwondolei jinai yeyote aliyehusika." Kafulila ambaye ndiye aliyeibua kashfa hiyo bungeni, aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa:

"Utaratibu huo ulikuwa kinyume cha sheria kwani jinai haifutwi kwa kurejesha ulichopora. Uamuzi wa Ngeleja ni hatua ya kwanza kwamba amekubali jinai na amerudisha na hivyo wenzake pia warudishe ili wabaki na jinai ya kwanini walijipatia fedha hizo vizivyo halali."

Alisema uamuzi wa kuwataka wahusika kulipa kodi ulifanyika baada ya presha ya Bunge baada ya kubaini hawakuilipa walipopata mgawo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Ngeleja alisema amerejesha mgawo huo pamoja na sababu nyingine, ili kujiweka kando na kashfa.

Wakili wa kujitegemea, Jeremia Mtobesya, akizungumza na Nipashe iliyotaka kujua uzito wa urejeshaji fedha kwa ujumla katika tuhuma za upokeaji kwenye makosa ya jinai juzi, alisema inategemea mashtaka yatahusu nini na kipengele gani cha sheria kitatumika.

Mtobesya alisema bado kuna jinai katika urejeshaji kwa mtuhumiwa anayedaiwa kupokea fedha isivyo halali lakini "kwa upande mwingine wanaorejesha inaweza kuwa nafuu kwao."

Wakili Mwandamizi wa Serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa sababu za kinidhamu, alisema urejeshaji unaweza kumsaidia mtuhumiwa kutegemeana na makubaliano kati ya Jamhuri na mrejeshaji husika.

"Hapo inategemea na makubaliano kati ya pande zote mbili... serikali na mtu mlipaji," alisema Wakili wa Serikali huyo.

Ngeleja alisema zaidi kuwa alipokea fedha hizo kama wabunge wengine na hakujua kwamba Rugemalira angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha za akaunti ya Escrow kama ilivyo sasa.

"Nimesononeshwa na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma," alisema Ngeleja.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive