Friday, 14 July 2017

MGHANA ATUA SIMBA


Kocha Joseph Omog.

KAIMU Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna, Jumanne iliyopita alienda nchini Ghana kwa ajili ya kumalizana na straika Thomas Agyei  raia wa nchi hiyo ili ajiunge na Simba kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi cha Simba.
Simba inamleta nchini straika huyo ili kuziba pengo la Frederic Blagnon  raia wa Ivory Coast  ambaye inatajwa kwamba klabu hiyo imepanga kuachana naye.

Taarifa za uhakika ambazo Championi Ijumaa imezipata kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, kigogo huyo wa Simba anatarajia kutua nchini leo Ijumaa akiwa na straika huyo baada ya kumalizana naye.
“Kajuna amefanikiwa kuweka mambo safi, kama unavyojua hivi karibuni alienda Ghana kwa ajili ya kumalizana na straika huyo ambaye tunamtaka kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi kutokana na pendekezo la benchi la ufundi chini ya kocha Joshua Omog.

“Kwa hiyo kesho (leo) ndiyo anarudi nchini akiwa na mchezaji huyo tayari kwa kuanza kazi yake ya kuitumikia Simba katika michuano ya ligi kuu msimu ujao.
“Sifa zake tulizopewa ni kwamba ni mshambuliaji mzuri kwa hiyo matarajio yetu ni kumuona akifanya vizuri uwanjani kwa ajili mafanikio ya klabu yetu,” kilisema chanzo cha habari.

Alipotafutwa Kajuna katika namba zake zote za simu ili kujua ni muda gani atatua nchini hakuweza kupatikana kutokana na kutokuwa hewani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive