BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa
waraka kwa wafanyabiashara wa maduka ya kuuza na kununua fedha za kigeni
kuomba upya leseni kwa ajili ya kufanya biashara hiyo. Leseni zote za
maduka ya kubadilisha fedha za kigeni zitafutwa ifikapo Septemba 2,
mwaka huu ili wamiliki waombe upya.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Msimamizi
Maduka ya Kuuza na Kununua Fedha za Kigeni wa Benki Kuu ya Tanzania,
Kanuti Mosha kwenye Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam (DITF) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara
ya Kilwa, Temeke jijini Dar es Salaam.
Mosha alisema kwa sheria ya sasa,
mfanyabiashara atatakiwa kumiliki duka moja tu tofauti na ilivyokuwa
awali mtu mmoja anaweza kumiliki maduka hata matano. Alisema sambamba na
kutoa leseni upya, BoT imeweka viwango vipya vya mtaji ambavyo
vinaanzia Sh milioni 100 hadi 300 kwa daraja A, na kuanzia Sh milioni
250 hadi Sh bilioni moja kwa daraja B na Amana ya Thamani kuanzia Dola
za Marekani milioni 50 hadi milioni 100.
Aidha, alisema wafanyabiashara wa Daraja B
watafanya miamala ya papo kwa hapo pamoja na miamala ya nje ya nchi.
Hata hivyo, Mosha alisema mbali na masharti ya mtaji, watahitajika pia
kufunga kamera tatu ‘CCTV‘ kwa ajili ya usalama.
Alieleza kuwa lengo ni kudhibiti
ubadilishaji wa fedha na utoaji wa stakabadhi, kamera zinatakiwa
kufungwa kaunta, kwenye kabati la kuhifadhia fedha na eneo la kuhudumia
wateja.
Alisema watakaokamilisha masharti hayo
ndio watakuwa wanaendesha biashara hiyo kuanzia Septemba mwaka huu
Wafanyabiashara hao wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni wamepewa
miezi mitatu kuanzia Juni 2, 2017 hadi Septemba mosi, mwaka huu
wakamilishe usajili na kumiliki duka moja tu. Mosha alisema endapo
mfanyabiashara atataka kufungua tawi, itamlazimu kutuma maombi BoT.
Chanzo: HabariLeo
0 comments:
Post a Comment