Tuesday, 11 July 2017

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMGONGA TWIGA



DEREVA wa basi la abiria la AM Coach, Andrea Jafari (42) amefi kishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kwa kosa la kuumua twiga anayekadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 33 baada ya kumgonga kwa uzembe.


Mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa mkoani Tabora alifikishwa jana mbele ya Hakimu wa wilaya hiyo, Teotimus Swai ambako alikana kosa hilo hivyo hakimu aliamuru arudishwe rumande hadi Julai 14, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Jafari amerejeshwa rumande baada ya kushindwa kukidhi vigezo vya dhamana ambavyo vilimtaka aache mahakamani hapo nusu ya thamani ya twiga aliyetuhumiwa kumuua ambayo ni zaidi ya Sh milioni 16.5, na pia awe na hati ya mali isiyohamishika ambayo imethibitishwa na mtathmini yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 16.5.

Aidha, mahakama hiyo ilimwamuru asalimishe hati zake za kusafiria na endapo akikidhi vigezo hivyo vya dhamana, asitoke nje ya Wilaya ya Mlele bila idhini ya mahakama. Kwa mujibu wa hakimu Swai, mshitakiwa huyo anashtakiwa kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria Namba 148, (5) (b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama iliyofanyiwa Marekebisho 2002, pia kifungu cha 146 cha sheria hiyo.

Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Baraka Hongori alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Aprili 18, 2017 saa mbili asubuhi ambako akiendesha basi la abiria akiwa katika mwendo wa kasi, alimgonga twiga katika miinuko ya milima ya Kanono iliyopo katika Pori la Hifadhi la Rukwa – Lukwati wilayani Mlele.

Alidai mshtakiwa huyo baada ya kumgonga na kumuua twiga huyo, alikimbia kusikojulikana hadi Julai 8, mwaka huu alipokamatwa mkoani Tabora na kurejeshwa Mlele.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive