Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Jumatano wiki hii, amezindua viwanda vikubwa vitatu na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam ikiwa ni siku yake ya pili ya ziara ya kikazi ya siku 3 mkoani Pwani.
Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha
Global Packaging Tanzania Ltd kilichopo katika eneo la viwanda Kibaha
ambacho kina uwezo wa kutengeneza mifuko ya sandarusi 53,000 kwa siku
kwa ajili ya kuhifadhia mazao.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na
Mtanzania Bw. Joseph Otieno Wasonga kimeajiri wafanyakazi 110 na
kimejengwa kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 8.
Pili, Rais
Magufuli amezindua mradi wa kutengeneza matrekta 2,400 aina ya Ursus
ambao utagharimu Shilingi Bilioni 55, na matrekta hayo yatasambazwa nchi
nzima kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo.
Mradi huu unamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na
utazalisha matrekta ya aina 6 zenye nguvu ya kuanzia HP50 hadi HP 85.
Tatu,
Mhe. Rais Magufuli amezindua kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group
kilichopo Mlandizi ambacho katika awamu hii ya kwanza kina uwezo wa
kuzalisha tani 500,000 za nondo kwa mwaka na awamu ya pili kitaongeza
uzalishaji hadi kufikia tani 1,200,000 kwa mwaka.
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amesema kiwanda
hicho kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania Bw. Mohamed Said Kiluwa
kwa asilimia 51 na asilimia 49 zinamilikiwa na mwekezaji kutoka China
ni muendelezo wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya China na
Tanzania.
Aidha, Shirika la Reli Tanzania (TRL) limejenga njia ya
reli ya kilometa 3.5 inayounganisha kiwanda hicho na reli ya kati ikiwa
ni juhudi za kurahisisha usafirishaji wa malighafi na vyuma
vinavyozalishwa kiwandani hapo kwenda ndani na nje ya nchi.
Akizungumza
katika miradi hiyo, Rais Magufuli amepongeza uwekezaji huo na ameagiza
vyombo vinavyohusika kutoa vibali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hapa
nchini viondoe urasimu ambao umekuwa ukiwakatisha tamaa wawekezaji
kujenga viwanda.
Dkt. Magufuli ametoa wito kwa wamiliki wa
viwanda hivyo kujali maslahi na usalama wa wafanyakazi waliowaajiri,
amezitaka benki hapa nchini kujielekeza kufanya biashara na wananchi kwa
kuwakopesha mitaji wafanyabiashara na wajasiriamali badala ya kutaka
kufanya biashara na Serikali na ameiagiza Wizara ya Nishati na madini na
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vya chuma
vinatumia malighafi za hapa nchini kutoka Mchuchuma na Liganga.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezindua mradi wa upanuzi wa mtambo wa
maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu ya maji ya kutoka Mlandizi
hadi Dar es Salaam uliojengwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya
Shilingi Bilioni 200 ikiwa ni mkopo kutoka Serikali ya India.
Kabla ya Rais Magufuli kuzungumza na wananchi waliohudhuria sherehe
za uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu wa India Nalendra Modi ametoa
salamu kwa njia ya runinga ambapo amempongeza Rais Magufuli na Serikali
yake kwa kufanikisha mradi huo ambao utasaidia kuondoa kero ya uhaba wa
maji inayowakabili wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa miaka mingi na
kueleza kwamba mradi huo utaboresha maisha ya watu.
Katika salamu
hizo zilizowasilishwa na Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya,
Waziri Mkuu Modi ametangaza kuwa Serikali yake imepitisha kiasi cha Dola
za Kimarekani Milioni 500 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 1 ambazo
Tanzania itakopeshwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya maji katika maeneo
mbalimbali .
Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri
Mkuu wa India M Nalendra Modi kwa kutoa mkopo huo na amesema upanuzi wa
mradi wa maji wa Ruvu Juu pamoja na mkopo huo vinaendeleza na kuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria kati ya Tanzania
na India.
Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji
kujipanga vizuri kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji inayosuasua,
kudhibiti upotevu na wizi wa maji na kuwakatia maji wadaiwa sugu wote.
Rais
Magufuli atakamilisha ziara yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani Pwani kwa
kuzindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drinks Ltd, kuzindua
kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kuzindua mradi
wa barabara ya Bagamoyo - Msata.
0 comments:
Post a Comment