Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa
kuwaua wahalifu wanne wanaosadikiwa kuwa miongoni mwa wahalifu
wanaoendesha mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji katika
mapambano yaliyodumu kwa zaidi ya nusu saa katika kijiji cha Pagae
wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Akielezea tukio hilo Mkuu wa Oparesheni
Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Liberatus Sabas
alisema tukio hilo lilitokea siku ya Alhamisi juni 29 majira ya saa tatu
usiku kwenye barabara ya vumbi itokayo Pagae kuelekea Nyambunda ambapo
Askari Polisi wakiwa doria walikutana na kikundi cha watu
kinachokadiriwa kuwa na watu sita ambapo wahalifu hao baada ya kuona
gari la Polisi walikimbilia vichakani na kuanza kuwarushia risasi
Polisi.
Sabas alisema baada ya hali hiyo
kutokea Askari nao kwa ujasiri walijibu na mapambano hayo yalidumu kwa
zaidi ya nusu saa ambapo Polisi walifanikiwa kuwajeruhi wahalifu wanne
kwa risasi ambao baadaye walifariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali.
“Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata
silaha mbili aina ya SMG na magazine mbili pamoja na risasi 17
zilizokuwa zinatumiwa na wahalifu hao na hii ni dalili kuwa tunaendelea
vizuri na oparesheni yetu ambayo inashirikisha vyombo vingine vya ulinzi
na Usalama katika wilaya hizi tatu za Mkuranga, Kibiti, na Rufiji” Alisema Sabas.
Aidha Sabas ametoa wito kwa wahalifu
wengine kuacha mara moja kufanya vitendo hivyo kwa kuwa vyombo vya
ulinzi na usalama vinaendelea kufanya jitihada zote za kuhakikisha kuwa
maeneo hayo yanakuwa salama na wananchi wanaishi katika hali ya amani na
usalama.
Vilevile amewataka wananchi kutoa
taarifa zitakazowezesha kupatikana wahalifu wengine ili kuhakikisha kuwa
kila mmoja anaishi kwa usalama ambapo kwa ambaye atakayetoa taarifa
zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu hao kiasi cha shilingi milioni
kumi kitatolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro.
Chanzo: ITV
0 comments:
Post a Comment