Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amefunguka kuwa wabunge wanaodai kuwa bunge ni dhaifu basi ni wazi watakuwa na mambo yanawasumbua ndio maana wanatoa kauli za kudhihaki chombo hicho.
Mhe. Ndugai amesema hayo leo mjini Dodoma baada ya kuwepo kwa baadhi ya wabunge wanaotoa kauli zisizokuwa rasmi katika vikao vya bunge bila kufikiria kwamba wanachokifanya hakina taswira nzuri kwa wapiga kura wao pamoja na kwa serikali kwa ujumla.
"Yupo mwenzetu alisimama hapa na kulalamika kuwa bunge hili ni dhaifu, kwa maoni yangu hizi ni lugha za kuudhi kwa sababu wenzako wengi namna hii waliochaguliwa na watu wakaletwa hapa halafu wewe unawaona kwa wingi wao ni dhaifu haipendezi. Unajua sisi tunaokaa hapa mezani hatuchangii kama nyinyi, kazi yetu ni kuwapa nafasi mseme, wakati mwingine zinatoka shutuma ambazo hatuna nafasi ya kubishana au kulumbana lakini wakati mwingine ni vizuri kutumia fursa hizi kusafisha baadhi ya mambo. Binadamu ni lazima uwe na staha ile ndogo tu kuwaheshimu binadamu wenzako," alisema Ndungai
Pamoja na hayo, Ndugai ameendelea kwa kusema "Katika bunge letu kinacholeta matatizo humu ndani ni tabia na lugha, tukirekebisha hayo mawili tutaenda vizuri tu lakini najua kundi hili ni kubwa hatuwezi kuwa wote tupo sawa, nitaendelea kulisemea lakini pale kwenye ulazima tutachukua hatua," alisisitiza Ndugai.
0 comments:
Post a Comment