Friday, 30 June 2017

KOREA KASKAZINI YAIPONZA CHINA

China imeghadhabishwa sana na hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo benki moja ya China ambayo inatuhumuwa kuhusika katika utakatishaji wa fedha za Korea Kaskazini.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya taifa hilo ameitaka Marekani "kukoma kuchukua hatua zisizo sahihi" kuepusha kudhuru ushirikiano baina ya nchi hizo.
Marekani ilitangaza hatua hiyo, pamoja na vikwazo dhidi ya kampuni ya uchukuzi wa meli ya China na raia wawili wa China mnamo Alhamisi.
Ilisema lengo la vikwazo hivyo ni kupunguza fedha ambazo Korea Kaskazini inaweza kutumia kuendeleza mpango wake wa kustawisha silaha.
"Tutafuatilia pesa hizo na kufunga mirija," Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin aliambia kikao cha wanahabari.

Hata hivyo alisema hatua hiyo haijatokana na China kutoichukulia hatua Korea Kaskazini, na kusema: "Hii hailengi China, hii inaangazia benki, pamoja na watu binafsi na mashirika yaliyopo China."
Umoja wa Mataifa ulikuwa tayari umeiwekea Korea Kaskazini msururu wa vikwazo, lakini China inatazamwa na wengi kama taifa lililo na uwezo zaidi wa kuiyumbisha Korea Kaskazini kupitia vikwazo vya kiuchumi.
Washington imekuwa ikiishinikiza Beijing kuchukua hatua kali zaidi hasa kutokana na hatua ya Pyongyang ya kufanyia majaribio makombora ya masafa marefu.
Lakini kupitia Twitter mapema mwezi huu, Rais Donald Trump alisema hatua ambazo China imechukua kufikia sasa hazijatosha.

Vikwazo hivyo vilitangazwa huku Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in akizuru Washington kwa mashauriano na Bw Trump kuhusu masuala ya usalama.
Vikwazo hivyo vina maana kwamba Benki ya Bandong sasa imepigwa marufuku kufanya biashara Marekani.
Wizara ya Fedha ya Marekani imesema benki hiyo imetumiwa kusafirisha na kutakatisha fedha za Korea Kaskazini na kwamba mamilioni ya dola ya pesa zilizolipwa kampuni zilizohusika katika mpango wa silaha za Korea Kusini zilipitishiwa katika benki hiyo.
Raia wawili wa China, ambao wanatuhumiwa kuunda kampuni ambazo zimekuwa zikitumiwa na mashirika ya Korea Kaskazini na kampuni moja ya uchukuzi wa meli ya Dalian Global Unity Shipping, zimedaiwa kuingiza kinyemela bidhaa hadi Korea Kaskazini, na zimewekewa vikwazo.
Bw Mnuchin amesema kwamba Marekani inaweza kuongeza vikwazo zaidi hivi karibuni.
Vikwazo hivyo vimetangazwa muda mfupi baada ya Marekani kutangaza mauzo ya silaha za thamani ya $1.42bn (£1.09bn) kwa Taiwan, shughuli kama hiyo ya kwanza kabisa ya kibiashara chini ya tutawala wa Trump.
Mauzo ya silaha kwa Taiwan kila mara kuiudhi Beijing kwani China huchukulia kisiwa hicho kinachojitawala kuwa sehemu ya himaya yake.
Kupitia taarifa, ubalozi wa China mjini Washington uliitaka Marekani kubatilisha hatua hiyo na kusema kuwa China ina kila haki ya kukasirika.
Wizara ya mambo ya nje ya China ilisema Ijumaa kwamba hatua ya Marekani ilienda kinyume na "moyo muhimu) wa urafiki kati ya Bw Trump na Rais wa China Xi Jinping waliouonesha walipokutana jimbo la Florida, Marekani mwezi Aprili.
Mapema wiki hii, Marekani pia iliiorodhesha China miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu duniani na kufanyiwa kazi kwa watu kwa lazima - hatua ya kwanza kabisa kuu ya utawala wa Trump dhidi ya China na haki za kibinadamu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive