Thursday, 20 April 2017

MAMA TUA NDOO YA MAJI KICHWANI-DAWASCO



Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo (wa kwanza kulia) akiwa ameambatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja (wa kwanza kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Archard Mutalemwa (katikati) kuelekea katika chumba cha mkutano baada ya kuwasili makao makuu ya Dawasco jana kupokea taarifa ya huduma ya maji jijini Dar es Salaam na Pwani.

Na Denis Massawe
Kampuni ya Usambazaji wa Maji Dar es Salaam (DAWASCO), pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) zimeonesha nia ya kuhakikisha kila raia anapata maji bila tatizo ili kufikia malengo ya Serikali katika kuwatumikia wananchi wake kwa kuwapa huduma za msingi.

Dawasco na Dawasa walionesha dira hiyo baada ya kutembelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo, katika ofisi zao zilizopo Posta jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka, Profesa Kitila Mkumbo alibainisha kuwa licha ya mafanikio makubwa waliyopata lakini bado wanachangamoto kubwa upande wa maji safi na maji taka lakini kwa miaka michache wamefanya vizuri.

Prof. Kitila alibainisha kuwa katika wizara zote serikalini Dawasco ndio inaongoza kwa makusanyo makubwa nchi nzima.
  
Katibu huyo mkuu alisema kuwa; “Pamoja na kazi nzuri mnayofanya ya kuhakikisha upatikanaji wa maji hakikisheni mnaongeza kasi ya usambazaji wa huduma hii muhimu kwa wananchi, kwakufanya hivyo mtakuwa mnatendea haki dhana ya kuwa mnaongoza kwa mapato lakini pia mnatoa huduma stahiki kwa wananchi.”

Profesa Kitila alibainisha kuwa kuwa licha ya ongezeko la upatikanaji wa maji, ipo changamoto ya idadi kubwa ya wananchi kutofikiwa na huduma hivyo ni lazima sasa Mamlaka husika kuongeza kasi ya usambazaji wa miundombinu ya maji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

Aidha Profesa Kitila alitoa rai kwa wateja wote wa Dawasco na Dawasa zikiwemo taasisi za umma kutii agizo la Mhe. Rais kwa kulipia huduma wanazopatiwa ili kuziwesha mamlaka hizo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Ambapo katibu huyo mkuu wa Idara ya maji na umwagiliaji alifafanua kuwa ameshuhudua ripoti ya shirika hilo ikionesha jinsi wananchi wanavyolipa fedha ya maji sasa iweje taasisi nyingine zisilipe? Alihoji Kitila na kusema kuwa; “ile meseji ya rais ya kukatia umeme watu wasiolipa haikuwa kwenye umeme tu na huku, kwenye kulipa isitokee Extension taasisi zote zilipe bili.”

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji wa Maji Dar es Salaam (DAWASCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema kuwa katika kuhakikisha uzalishaji wa maji umeongezeka kwa kutoka lita za ujazo wa mita 160 Milioni kwa siku hadi kufikia lita za ujazo mita 271Milioni kwa siku ambazo ni sawa na asilimia 100.37% ya lengo la upatikanaji wa maji ambalo ni lita 270 Milioni kwa siku.

Mhandisi Luhemeja aliongeza kuwa jumla ya Vizimba 560 (Gati za kuuzia maji) vimeunganishwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi ikiwa ni muendelezo wa kuongeza kasi ya usambazaji na upatikanaji wa huduma ya maji miongoni mwa jamii.

Katika hatua nyingine Afisa Mtendaji Mkuu huyo alisema kuwa katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuhakikisha wakina mama wanatua ndoo za maji kichwani Dawasco inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa kuongeza usambazaji wa huduma ya maji katika eneo la takribani 1,427Km unaohusisha maeneo ya Tegeta, Mpiji hadi Bagamoyo ifikapo mwezi Julai mwaka huu ambapo tayari fedha Tsh. 117Bilioni kwa ajili ya mradi huo zimepatikana kupitia Benki ya Dunia, mradi huo utakapokamilika unakadiriwa kuongeza idadi ya watumiaji wa maji takribani laki moja.

Mhandisi Lumeja alisema kuwa; “Katika kuhakikisha inafikia azma ya kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi Dawasco inaendesha Kampeni ijulikanayo ‘Mama Tua Ndoo ya Maji Kichwani Ndani ya Siku 90’ ikiwa na lengo la kuwaunganisha na huduma ya maji wateja takribani 151,000 wataunganishwa na huduma hiyo katika eneo linalopakana na Barabara ya Morogoro, Kampeni hiyo imeanza kuanzia tarehe 1 Aprili hadi 30 Juni, 2017.”

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka jijini Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Archad Mutalemwa, alibainisha kuwa  mipango yao kwa sasa ni  kupanua mtambo wa Ruvu chini, upanuzi wa mtambo wa Ruvu juu pamoja na kuchimba visima 20 na awamu itakayofuata watachimba visima 30.

Ambapo alidai kuwa mpaka kukamilika kwa miradi hiyo hitagharimu kiasi cha Trilioni 2.2 huku akisema kuwa wanatarajia kuanza ujenzi wa bomba jipya toka Ruvu hadi Dar es Salaam.

Iicha ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) kuainisha miradi hiyo itakayomuezesha mama kutua ndo ya maji kichwani, imejiimarisha pia katika hutoaji huduma ya makusanyo na usambazaji maji kwa kuwapa elimu watendakazi wake.

Miongoni mwa semina zilizofanywa na Mamlaka hiyo kwa lengo la kutoa elimu ni ile ya mwaka jana iliokuwa na lengo la kuwataka viongozi wa Jumuiya za watumia maji katika jiji la Dar es salaam na baadhi ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani kusimamia kikamilifu mapato na matumizi ya miradi ya maji ili kuepuka migogoro inayosababishwa na matumizi mabaya ya fedha jambo linalochangia baadhi ya miradi kushindwa kujiendesha na kuwa kero kwa wananchi.

Semina hiyo iliongozwa na Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka hiyo Bi.Neli Msuya, wakati akitoa elimu kwa viongozi hao kuhusu uendelezaji wa miradi inayosimamiwa na Jumuiya 15 za Watumia Maji zilizojengwa chini ya mradi wa Maji Yetu kwa ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji.

Meneja huyo alibainisha kuwa Dawasa imekukutana viongozi hao kuwakumbusha wajibu walio nao katika kuhakikisha miradi wanayoisimamia inakidhi matarajio ya wananchi kwa kutoa huduma bora na kujiendesha kwa faida na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Kwa kuzingatia idadi ya watu zaidi ya Laki mbili (200,000)  wanaohudumiwa na mradi huu kwa kupata maji safi na salama na gharama kubwa iliyotumika kuanzisha mradi huu shilingi Bilioni 14.5 ,tumeona kuna umuhimu wa kuendelea kuweka msisitizo wa uangalizi kwa kuwa miradi hii ni muhimu na iko kwa wananchi.” alisisitiza.

Bi Nell alifafanua kuwa majukumu ya Dawasa kama mmiliki wa miundombinu ya majisafi na majitaka ni kugharamia matengenezo makubwa na kufanya uwekezaji wa kupanua miundombinu ya majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam na maeneo yaliyoainishwa chini ya Sheria ya Dawasa Namba.20 ya Mwaka 2001.

Dawasa iliingia mkataba wa uendeshaji na Shirika la Maji safi na Maji taka Dar es salaam (DAWASCO) kutoa huduma ya uondoshaji wa maji taka katika jiji la Dar es salaam, Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.
kupitia mkataba huo,  Dawasco huuza maji kwa wateja, kutayarisha Ankara za maji, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji na kufanya matengenezo ya mfumo mzima wa usambazaji maji na uondoshaji majitaka katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.

Meneja huyo alisema kuwa; “Kupitia elimu inayotolewa leo mtagundua kuwa ninyi ni muhimu katika kuwahudumia wananchi, mtaona kuwa ninyi ni DAWASCO ndogondogo kwenye maeneo yenu kwa kuwa mnauza maji kwa wateja, mnatayarisha Ankara za maji , mnakusanya fedha za malipo ya huduma mnafanya matengenezo ya mifumo ya maji kwa wateja wenu” Amesisitiza.

Kwa sasa Dawasa imewekeza kwenye miradi mikubwa na kupanua chanzo cha Maji cha Ruvu chini ambacho huzalisha lita milioni 270 kwa siku, ujenzi wa Bomba kubwa lenye urefu wa Kilometa 56 kutoka Ruvu Chini hadi matenki yaliyopo chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.

Kwa upande wa Ruvu juu maboresho makubwa yamefanyika kwa kupanua mitambo ya uzalishaji ambayo sasa itazalisha lita milioni 196 kutoka milioni 82 kwa siku.

Upande wa maeneo ya kaskazini na kusini mwa jiji la Dar es salaam kuelekea wilaya ya Mkuranga Dawasa inaendelea kuwekeza katika uchimbaji wa visima virefu vya maji na kuweka mifumo ya usambazaji wa maji ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama kwa gharama nafuu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive