Monday 16 January 2017

WAZIRI MKUU AWAPINGA WAODAI UWEPO WA BAA LA NJAA


Waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa amezisoma habari kwenye vyombo mbalimbali vya Tanzania zikisema kwamba nchi hii imekumbwa na baa la njaa.
Baada ya kuzisoma zote hizo ameyasema yafuatayo >>> Tanzania haijakumbwa na baa la njaa, Watanzania wasisikilize kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la  kupandisha bei za vyakula.
Akiwa Dodoma leo Jumatatu Januari 16, 2017 amesisitiza >>> “mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni 3 na ikafanya baadhi ya Wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi na serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula,”
Amesema baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na tani milioni 1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini.
“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” – Waziri mkuu Majaliwa
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali hivyo Wananchi wazitumie kwa kulima mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame na endapo kutatokea uhaba wa chakula nchini, serikali itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri mkuu imemalizia kwa kusema kuhusu kupanda wa bei ya vyakula katika baadhi ya masoko kumetokana na kuwepo kwa uhaba wa chakula katika nchi jirani na kwamba Wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi, itatoa taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula kwa sasa na pia itatoa taarifa kuhusu hali ya mvua ili Watanzania wapate ukweli wa hali ilivyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive