Friday 6 January 2017

SERIKALI INAWAJIBIKA KUMTAFUTA BEN SAANANE- LISSU


MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, amesema serikali ndiyo yenye wajibu wa kumtafuta na kumpata raia wake, Ben Saanane,  ambaye amepotea kwa miezi ipatayo miwili sasa.

Lissu ameyasema hayo wakati akizungumza na Global TV Online inayomilikiwa na kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa magazeti ya Uwazi, Championi, Ijumaa, Risasi, Amani na  Ijumaa Wikienda.

Mwanasheria huyo alikuwa akijibu swali kuhusu ukimya wa chama chake kuhusu kada wake huyo ambaye amezua tafrani nchini akiwa hajulikani akiwa hai au amekufa.

Alikanusha uvumi unaoenezwa kwamba huenda chama chake kinahusika katika kupotea kwa  mtu huyo, ambapo alisema katika kukwepa kusema kitu kisichojulikana, wameitaka  serikali kutoa tamko iwapo inafahamu Mtanzania huyo aliko au haifahamu.

lissu-global-tv-10“Mpaka sasa serikali haijasema lolote kuhusiana na jambo hilo.  Tunafahamu Ben amepotea lakini wakati mwingine tunanyamaza kwa sababu tunachokifahamu sisi ni sawa na mnachokifahamu nyie (waandishi wa habari) ila nawahakikishia kwamba hatuhusiki kwa vyovyote na kupotea kwake,” alisisitiza mwanasheria huyo machachari.


Akisisitiza msimamo wa chama chake, alizitaka mamlaka zote husika na usalama wa raia ziseme hali halisi inayozingira sintofahamu ya mahali alipo Saanane ikiwa yuko ndani au nchi za nje, au hata kama amefariki na kuzikwa kwa kutotambuliwa.


Akizungumza kuhusu kutoonekana kwake huko Arusha kusaidia juhudi za kumpatia dhamana Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, mwanasheria huyo alisema kuna wanasheria wengi wa chama hicho wanaoweza kufanya kazi hiyo lakini akasema suala hilo linaonekana gumu kwa vile linaendeshwa kisiasa.


Hata hivyo, alisema ataungana na wanasheria wenzake ili kulipatia ufumbuzi suala hilo linaloonekana kuendelea bila sababu za msingi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive