Friday 6 January 2017

MWIGIZAJI MKONGWE NCHINI INDIA OM PURI AFARIKI DUNIA


 Om Puri aliigiza katika filamu India, Uingereza na Marekani

Mwigizaji mashuhuri nchini India Om Puri, ambaye pia aliigiza kwenye filamu zilizovuma sana nchini Uingereza, amefariki dunia akiwa na miaka 66.

Om Puri aliigiza kwenye filamu ya ucheshi ya East is East nchini Uingereza ambayo ilisimulia kuhusu maisha ya mhamiaji kutoka Pakistan aliyekuwa akizoea maisha kaskazini mwa England.

Taarifa zinasema mwigizaji huyo alifariki baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo nyumbani kwake Mumbai mapema Ijumaa.

Om Puri alijulikana sana kwa ustadi na uigizaji wake katika filamu za Kihindi miaka ya 1980.

Aidha, aliigiza kwenye filamu za Kiingereza, zikiwemo Mahatma Gandhi ya Richard Attenborough.
Aliigiza pia katika filamu za Pakistan na Hollywood.

Mwaka 2004, alitunukiwa nishani ya staha ya OBE kwa mchango wake katika tasnia ya filamu Uingereza.

Puri, alizaliwa 1950 jimbo la Haryana, kaskazini mwa India.
 Om Puri akiwa na mwigizaji Helen Mirren katika The Hundred-Foot Journey

Filamu yake ya kwanza kuigiza ilikuwa ya Ghashiram Kotwal mwaka 1976.

Nchini India, anafahamika kwa filamu maarufu za Ardh Satya, Sadgati, Paar na filamu ya ucheshi ya Jaane Bhi Do Yaaro.

Majuzi, alizungumzia marufuku iliyotolewa na India kwa waigizaji wa Pakistan kutokana na kuongezeka kwa uhasama kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.

"Waigizaji wa Pakistan si magaidi," aliambia runinga moja India, hatua iliyomfanya kushutumiwa na baadhi ya vyombo vya habari India.
Om Puri aliigiza katika kipindi cha runinga cha BBC cha The Canterbury Tales akiigiza kama Jetender
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive