Thursday 5 January 2017

MAUZO YA KITABU CHA ADOLF HITLER YATIKISA UJERUMANI

 
 Mafisa wa taasisi iliyochapisha upya kitabu cha kiongozi wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler cha Mein Kampf (Mapambano au Mapigano yangu) wamesema mauzo ya kitabu hicho yaliongezeka sana tangu kuanza kuuzwa kwa kitabu hicho Januari 2016.
Nakala 85,000 za kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kijerumani zimeuzwa katika kipindi hicho cha mwaka mmoja.
Mkuu wa Taasisi ya Historia ya Kisasa (IfZ) iliyochapisha kitabu hicho Andreas Wirsching amesema mauzo hayo yamewashangaza sana.
Hata hivyo, bado hakijafikia vitabu vingine vilivyouzwa zaidi nchini Ujerumani.
Nakala ya kitabu hicho huuzwa €58 (£49).
Kitabu hicho kinachoangazia sera aliyoifuata Hitler kilikuwa mwongozo wa utawala wa Nazi. Hitler, kwenye kitabu hicho, alieleza wazi chuki dhidi ya Wayahudi.
Kitabu hicho kilipigwa marufuku baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na serikali ya Bavaria, ambayo ilimiliki haki za kitabu hicho.
Hii iliwazuia watu kuchapisha au kusambaza kitabu hicho kwa miaka 70.
Kwa mujibu wa Sheria Ujerumani, hakimiliki hudumu kwa miaka 70 na baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, IfZ ya Munich iliweza kuchapisha kitabu hicho na kuanza kukiuza Januari mwaka 2016.
Tofauti na vitabu vilivyochapishwa wakati wa utawala wa Nazi, nakala za Mein Kampf za IfZ zina jalada la rangi nyeupe ambayo haina picha ya Hitler.
Swastika na nembo nyingine za Nazi ni marufuku Ujerumani.



Inakadiriwa kwamba nakala 4,000 za kitabu hicho ziliuzwa Ujerumani mwaka 2016.
Hatua ya kuchapisha upya kitabu hicho ilishutumiwa vikali na makundi ya Wayahudi, yanayodai kazi za Sanaa za Nazi hazifai kuendelezwa.
source BBC
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive