Monday, 23 January 2017

LIPUMBA ANUSURIKA KIPIGO KWA VIJANA WA UKAWA BAADA YA KUKIMBILIA MSIKITINI


MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amenusurika kupigwa na vijana wanaoaminika kuwa ni wa Ukawa wakati akitoka kwenye mkutano wa kampeni mjini Morogoro.

Katika vurugu zilizotokea juzi jioni wakati vijana wa Ukawa na kikundi cha ulinzi cha CUF (blue guard) cha Dar es Salaam wakiwa na Profesa Lipumba walikuwa wakitoka kwenye mikutano ya kampeni maeneo tofauti walipokutana barabarani na kuanza kurushiana maneno na hatimaye kupigana.

Katika vurugu hizo, vijana wa Ukawa waliwazidi wenzao wa blue guard na Profesa Lipumba kulazimika kukimbilia kwenye Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja ili kujinusuru.

Ghasia hizo zilizodumu kwa takribani saa moja na nusu ambapo baada ya Profesa Lipumba kukimbilia msikitini hapo, wafuasi wa Ukawa walibaki nje mpaka polisi walipofika na kuwatawanya.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alikiri kutokea kwa vurugu hizo ambapo alisema wafuasi watatu wa CUF walijeruhiwa.

Alisema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini walioanzisha vurugu hizo ikiwa ni pamoja na kuweka doria kali katika mikutano ya vyama vya siasa.

Profesa Lipumba hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake kutokuwa hewani jana.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive