ZIMESALIA siku nne tu Rais wa Marekani, Barack Obama, kung’atuka madarakani.
Rais huyo anatarajia kumkabidhi Ikulu ya Marekani Rais mteule, Donald Trump, Ijumaa wiki ijayo.
Kabla ya tukio hilo kufanyika hivi karibuni Rais Obama alitoa hotuba ya kuaga taifa hilo akiwa mjini Chicago, nchini humo.
Kama kawaida yake, aliongea kwa pozi, sentensi moja na nyingine zilitawaliwa na tuo, alivuta pumzi, akatuliza kichwa.
Midomo yake ilitamka maneno yanayowavuta wapigakura, wanasiasa, viongozi na zaidi kuvuta usikivu miongoni mwa wanajamii.
Obama alikuwa yuleyule wa mwaka 2004 alipotikisa nchi hiyo alipokuwa
Seneta Illinois. Obama alikuwa yuleyule wa mwaka 2008 akiomba ridhaa ya
kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Alikuwa Obama yuleyule jasiri na mwenye nguvu za hoja zilizomshinda
John McCain wa Republican wakati wa midahalo ya kuwania urais.
Alionyesha uimara wake wa kuivuta hadhira, maneno yake yalijaa hekima,
kiunganishi na kujenga umoja.
Na pengine ndiyo desturi ya Chama cha Democrat kuunganisha wananchi
na hata viongozi wa ulimwengu kuliko Republican wenye taswira kama ya
Donald Trump, George W. Bush mkubwa na George W. Bush mtoto au kina
Henry Kissinger na wengineo.
Ni Obama yuleyule aliyemshinda Mitt Romeny wa chama cha Republican mwaka 2012 katika kinyang’anyiro cha urais.
Alikuwa Obama aliyesimama imara, akajenga hoja, aliongea kama
kiongozi thabiti na mwenye kufurahia maisha binafsi ya kifamilia,
uongozi na jeuri ya kuzaliwa Marekani. Na huo ni upande wa mwonekano wa
mhutubiaji katika kuwasiliana na hadhira yake.
Katika hotuba yake kulikuwa na mambo mengi ambayo tunaweza kuyagawa
katika makundi ya vilio, furaha yenye kutia moyo, kusikitisha na mafunzo
kadha wa kadha katika anga za masuala ya siasa ulimwenguni hususani
uongozi na demokrasia.
Ni mafunzo ambayo yamekuwa adimu kutolewa kwa baadhi ya wanasiasa,
lakini Obama amedhihirisha kuwa bado kinara wa kuhamasisha, kutia moyo,
uwezo mkubwa wa ushawishi kwa wapigakura na zaidi anakuwa kiongozi wa
kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika kumaliza kipindi cha miaka 8
madarakani. Obama anaondoka akiwa na rekodi mbalimbali za kiutendaji,
ikiwemo mazuri na mabaya yake.
Mathalani kwenye hotuba yake alisema: “Baada ya miaka nane ya kuwa
rais wenu, bado naamini kwamba na ieleweke si suala la imani pekee bali
mapigo ya mioyo yetu Wamarekani, tumekumbatia uzoefu na mtindo wetu wa
kuunda Serikali ya kipekee kila mara.”
Nini tafsiri ya nukuu tuliyochukua? Ni dhahiri Obama anathibitisha
kuwa muundo wa Serikali na sera za Marekani zimekuwa za kipekee na dunia
imeshuhudia yote hayo.
Katika upande wa furaha Marekani imeleta mambo mengi yenye
kuheshimika kuanzia viunga vya Umoja wa Mataifa, hisa zake katika Benki
ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani ni miongoni mwa mashirika makubwa
ambayo yamekuwa yakitumiwa na mataifa mbalimbali kujipatia mikopo.
Aidha, muundo wa kipekee wa Marekani ni pamoja na kuileta dunia
katika ardhi yao. Wanaweza kuweka mikakati katika masuala ya ulinzi,
kulinda masilahi yao, kushikamana na mataifa rafiki na hata kuwa tayari
kupambana kwa silaha za moto ili kuhakikisha masilahi yao yanakuwa
kwenye mikono sana.
Anadhihirisha kuwa nchi yao imekuwa kwenye mkondo wa kuendesha mambo
inayoyataka kwa wengine bila bughudha na kuhakikisha mawazo yao ya
Kimarekani yanatawala dunia.
Hakuna biashara kubwa ambayo Marekani inafanya kama kuuza mawazo
yake. Biashara hii imekuwa muhimu na ndio msingi wa sera mbalimbali,
tangu ilipoiga hayo kutoka kwa wakoloni wa jamii za Ulaya hususani
Uingereza. Tukumbuke pia jamii za Uingereza nazo zilijikita kwa jamii za
Italia.
Sehemu nyingine anasema: “Kwa miaka 240, suala la ukazi wa wananchi
katika taifa letu limetupatia kazi na umuhimu wa kukiachia mafunzo
kizazi kimoja hadi kingine. Ni hicho kinachotuongoza, ni uzalendo wetu
tuliochagua kama taifa, kuanzia chipukizi hadi wakongwe, toka zama za
utumwa hadi ushujaa wa kutengeneza reli ya mafanikio ya nchi.”
Tafsiri ya nukuu hiyo ni kwamba, utaifa wa Marekani umeundwa
Kimarekani, ndio maana katika mitaala ya elimu hapa nchini tuliwahi
kufunzwa juu ya ubeberu wa Kimarekani (America Capitalism) ambayo
ilielezwa kuwa tofauti na ubeberu wa Uingereza (British Capitalism).
Sababu kubwa ni moja; Marekani walitafuta uhuru wao, wakatengeneza
mawazo yao, wakayauza kote duniani.
Kisha wakabuni silaha na vita kama bidhaa muhimu kwenye soko la
biashara. Maeneo mengi ambayo Wamarekani wapo yanakuwa na bidhaa mbili
kuu; silaha na vita.
Kwa wataalamu wa masuala ya siasa ya kimataifa wanaelewa ninachosema
kuwa silaha na vita ni miongoni mwa bidhaa muhimu mno kwenye mafanikio
ya nchi kama Marekani.
Mifumo yao ya uchaguzi ya kura za moja kwa moja za wananchi
(Electoral Vote) na kura za wajumbe wa majimbo (Electoral College) ni wa
kipekee ambapo iwapo mgombea hajapata kura nyingi za wajumbe
anaangushwa hata kama alipata kura nyingi za wananchi.
Ni mfumo wa kipekee wa Kimarekani, ndiyo ufahari wa Obama
anaozungumzia kwenye hotuba yake juu ya miaka 240 ya fikra za
Kimarekani.
Aidha, tumejionea vilio ambavyo Obama anaviacha duniani. Obama
anaondoka akiwa hajatatua suala la Afghanistan. Anaondoka akiwa Marekani
hajatatua suala la Irak.
Obama anaondoka akiwa ameshindwa kukamilisha mradi wa kuwakabidhi
wapinzani wa Rais Bashar Al Assad wa Syria. Katika mgogoro wa Syria
tumeshuhudia malumbano makali baina ya Urusi na Marekani, lakini
mwishowe Obama akaweka ‘silaha’ chini na kumwacha Vladimir Putin
akiibuka mshindi.
Obama anaondoka akiwa ameacha wingu la jeuri huko Libya, ambapo
Serikali yake ilishirikiana na majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi
(NATO) kumwangusha Rais Muammar Gaddafi.
Katika kipindi hicho, Obama alikaribia kuvunja sheria za nchi badala
ya kusubiri kuidhinishiwa jeshi la kwenda vitani kwa siku 60 kutoka
bungeni, lakini alikuwa tayari kuivunja.
Obama anaondoka katika kiti chake akiacha kilio cha Ukraine, ambao
wametibuana na jirani yake Urusi kutokana na sakata la Jimbo la Crimea.
Tumeshuhudia mapigano baina ya Ukraine na Urusi ambapo jimbo la Crimea
lilitaka kujiunga na kuwa sehemu ya Shirikisho la Urusi kuliko kuwa
sehemu ya Ukraine.
Obama ametuliza tu mgogoro wa silaha za nyuklia baina ya Iran na
Marekani pamoja na nchi za Magharibi. Mgogoro wa Georgia uliolipuka
zaidi Agosti mwaka 2008 dhidi ya Urusi haijamalizika.
Migogoro ambayo hajaimaliza licha ya kuingilia kati ni baina ya
Israel na mataifa ya Asia hususani Iran, Irak, Mamlaka ya Palestina na
Lebanon kwa kuzitaja chache. Ni mambo muhimu ambayo hakupaswa kuyaweka
kiporo.
Na sifa kuu ya mwisho ya Marekani itakuwa kumkabidhi madaraka, Donald
Trump kwa amani, tofauti na Yahya Jammeh wa Gambia anavyoshindwa
kutekeleza matakwa ya kisheria kumkabidhi Adama Barrow. Lakini je,
ufahari wa Obama kiuongozi na chozi lake juu ya hali ya Libya ni furaha
au kilio?
0 comments:
Post a Comment