TUKIO la kushangaza lililohusishwa na kifo cha Denis Komba (24) baada ya
nyoka aliyekuwa naye kuuawa, limechukua sura mpya baada ya mambo kadhaa
kuibuka.
Hayo ni pamoja na familia kudai mzoga wa nyoka na kwenda nao kuuzika
nyumbani, jambo lililoendelea kuhusisha suala hilo na imani za
kishirikina.
Imeelezwa kuwa familia ilielezwa na mganga wa kienyeji kuwa mwili
uliohifadhiwa hospitali, si wa mtoto wao, jambo lililowafanya kuuchukua
mzoga wa nyoka na kwenda kuuweka katika mfuko wa sarandusi (kiroba) na
kuuzika.
Hata hivyo, mashuhuda walieleza kuwa, familia hiyo ilikikata kichwa cha
nyoka na kukizika kivyake na kiwiliwili sehemu nyingine huku mwili wa
Komba ambaye naye alizikwa jana, ukizikwa katika kaburi eneo lingine
tofauti. Tukio hilo ni la juzi na lilimhusu Komba, mkazi wa Mateka,
manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Nyumbani kwao ni kilometa tano kutoka katikati ya mji wa Songea. Kabla
ya maziko, baadhi ya vijana waliokuwa wamebeba jeneza, walikuwa
wakikimbia nalo mwendo wa mchakamchaka huku wakiimba “mkimbize mkimbize
nyoka awahi asije kudhuru watu wengine”. Katika maziko hayo, hakuna
ndugu aliyeonekana kulia wala hakukuwa na ibada yoyote wakati jina la
marehemu linadhihirisha kuwa ni wa imani ya Kikristo. Wakati hayo
yakiendelea msibani, baadhi ya watu wake wa karibu walidai alikuwa na
tabia ya kucheza na nyoka mara kwa mara.
Hata hivyo, baba mzazi alikana kumuona mwanawe na nyoka. Naye daktari
aliyechunguza mwili, alisema kifo cha Komba kinatokana na kugongwa na
nyoka mwenye sumu kali, lakini hakuna jeraha wala alama yoyote
iliyoonekana katika mwili huo. #HabariLeo
0 comments:
Post a Comment