Home »
» NJIA 7 ZA UHAKIKA ZA KUPATA AJIRA HIZI HAPA
Kupata
nafasi za ajira imekuwa ngumu siku hadi siku, hususani ukitilia maanani
kuwa wahitimu wanazidi kuwa wengi na hali ngumu ya uchumi inafanya
waajiri kushindwa kuongeza nafasi mpya za kazi. Hakuna haja ya kukata
tamaa ya kupata kazi ile unayoitarajia hata kama kuna ukiritimba mwingi
katika soko la ajira kama vile watu kupeana kazi kwa kujuana, nafasi za
kazi kutotangazwa au kazi haipatikani mpaka rushwa itembee. Makala hii
inaenda kujadili mambo ya msingi kwa yeyote anayetafuta kazi, uwe kwa
sasa umeajiriwa unatafuta kazi mbadala au uwe hauna ajira unatafuta
ajira, bila shaka mambo yanayojadiliwa hapa yatakusaidia.
1. Mtazamo wako kuhusu ajira
Fahamu kuwa bidhaa ni chochote kile
ambacho kinatimiza mahitaji fulani. Mwenye kuhitaji bidhaa huwa anaitwa
mteja. Muajiri anatafuta mfanyakazi kwa kuwa analo hitaji la kazi
fulani kukamilika, na anayo matarajio kadhaa kutoka kwa mfanyakazi
anayemuajiri. Hivyo wewe kama mfanyakazi mtarajiwa unayo ‘bidhaa’,
yaani uwezo wako wa kutimiza majukumu fulani ambayo utatakiwa kufanya na
muajiri. Kwa hiyo mtazamo sahihi unaotakiwa kuwa nao wakati unatafuta
kazi ni kuwa wewe ni muuzaji wa bidhaa, na muajiri wako mtarajiwa ni
mteja. Kwa kuwa wapo ‘wafanyabiashara’ wengi wa hiyo bidhaa kama yako
(watu wanaotafuta ajira), unahitajika basi kujipanga vyema ili
kumshawishi na kumfanya mteja wako (muajiri mtarajiwa) aone kweli
sababu ya kununua ‘bidhaa’ kutoka kwako.
2. Wasifu wako ujitosheleze
Ukiwa na mtazamo ulioelezwa hapo juu wa
kuwa wewe ni mfanyabiashara unauza bidhaa kwa mteja wako (muajiri),
unatakiwa basi utumie vyema wasifu wako (CV) kujieleza vyema ili ‘mteja’
akukubali. Mambo ya kuzingatia katika wasifu wako ni kama yafuatavyo:-
Wasifu wako uendane na aina ya kazi
unayoomba; hivyo basi usiweke kila aina ya maelezo hata yale ambayo haya
umuhimu na kazi husika. Mfano unaomba nafasi ya kazi ya uhasibu, lakini
unaweka maelezo ya uzoefu wa sehemu tatu tofauti ya kazi za ulinzi.
Wasifu wako uoneshe kweli unao uwezo wa
kazi unayoiomba; hivyo basi usitaje tu majina ya kampuni au asasi
ulizofanya kazi na aina ya cheo ulichoshika ukiwa huko, bali eleza mambo
ya msingi ambayo ni mafanikio ya wewe kuwepo katika kampuni au asasi
fulani uliyokuwepo. Mfano kwa kazi yako kama msimamizi wa ofisi, uliweza
kuandaa mikutano (itaje) ambayo ilikutanisha watendaji wakubwa wa
kampuni yako ambapo kupitia maandalizi mazuri uliyoyafanya, kampuni yako
iliweza kupendekezwa mara tatu mfulululizo kuandaa mikutano hiyo.
Wasifu wako uoneshe utofauti wako wewe
na watu wengine; haitoshi kuandika katika CV yako kuwa umemaliza masomo
ya ngazi ya stashahada au shahada, haitoshi kutaja kuwa umewahi kufanya
kazi fulani mfano kazi ya usimamizi wa ofisi halafu ukaorodhesha
majukumu ya msimamizi wa ofisi, mambo ambayo kwa ujumla yanajulikana
kuwa ni majukumu ya msimamizi wa ofisi yeyote yule wa ofisi.
Kumbuka wasifu wako (CV) ni nyaraka
muhimu ya kumshawishi ‘mteja’ kuwa ananunua ‘bidhaa bora’ zaidi ya
nyingine katika soko la ajira. Hivyo basi jipange kwa kuonesha utofauti,
badala ya kutaja tu ngazi za juu za elimu ulizofanikiwa kufika, taja
pia maeneo ambayo wewe kweli ‘upo vizuri’ yaani maeneo ambayo kweli
haubabaishi katika ngazi hizo za elimu unazotaja. Pia kwa upande wa
uzoefu wa kazi, taja mafanikio uliyokwisha kupata kutoka ajira zako
zilizopita, au tuseme mambo gani ‘mazito’ ulikamilisha na kusaidia ukiwa
kwa waajiri wengine.
3. Fuata maelekezo kwa ufasaha
Unapowasilisha maombi yako ya ajira,
hakikisha unafuata maelekezo yaliyotolewa katika tangazo la nafasi za
kazi, kwani hata kama ni jambo dogo, utakalokosea linaweza kuchukuliwa
kama sababu ya wewe kutokuwa mfanyakazi makini, hivyo kukosa hata nafasi
ya kuitwa kwa usahili (interview).
Mfano kama umeambiwa uorodheshe
wadhamini watatu, hauna sababu ya kuorodhesha wadhamini wawili tu. Kama
umeambiwa utume maombi kwa njia ya posta, usitume maombi yako kwa barua
pepe wala kupeleka kwa mkono. Hakikisha pia unafuata maelekezo ya tarehe
na muda wa kuwasilisha maombi yako ya kazi. Pia zingatia maelekezo
kuhusu vyeti na nyaraka nyingine unazotakiwa kuziambatanisha pamoja na
barua yako ya maombi ya kazi. Kama umeambiwa utume CV yako tu,
usihangaike kutuma vitu vingine kama vyeti na barua ya maombi ya kazi.
SOURCE: MTEMBEZI
ITAENDELEA …
0 comments:
Post a Comment